SERA ya elimu ya mwaka 2014 imepata mafanikio makubwa kwa watoto wa kike baada ya mahudhurio ya wanafunzi wa kike kufikia asilimia 52 huku watoto wa kiume ikifikia asilimia 48.
Akizungumza katika kongamano la wanawake Kanda ya kusini lilofanyika mjini Songea, kuelekea maadhimisho ya siku wanawake duniani,Mwakilishi wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Hanifa Selengu amesema sera hiyo imetekelezwa na serikali ya Awamu ya tano kwa mafanikio makubwa.
Selengu amesema serikali imetenga kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 25 ili kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye haki ya kupata elimu anakwenda shule hali ambayo imesababisha uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari kuongezeka zaidi ya mara tatu.
“Wanataaluma wanasema watoto wa kike wanapoongezeka katika kupata elimu,uchumi wa nchi pia unaongezeka’’,alisema Selengu.
Kulingana na Mwakilishi huyo wa Wizara ya Afya,utekelezaji wa sera hiyo umezipa pengo la mahudhurio sawa ya elimu kwa watoto wa kike na kiume ambapo takwimu za BEST za mwaka 2018 zinaonesha kuwa katika shule za serikali wanafunzi wanaokwenda shule ni asilimia 6.9.
Hata hivyo amesema kitendo cha serikali kuondoa ada katika shule za serikali kumesababisha kuongezeka kwa wanafunzi katika shule za msingi kutoka 9.317,791 mwaka 2017 hadi kufikia wanafunzi 10,111,671 mwaka 2018.
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa kongamano hilo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amelitaja lengo la kongamano hilo kuwa ni kujadili kwa pamoja hali ya elimu katika kanda ya Kusini na umuhimu katika kuleta maendeleo endelevu.
Mndeme amesema kongamano hilo pia litajadili fursa za uongozi kwa wanawake na hali ya ukatili wa kijinsia katika jamii na kupanga mkakati wa kufikia maendeleo ya jamii endelevu.
Amesema serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kuhakikisha unatokomezwa pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
“Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto unatekelezwa kwa lengo la kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022’’,alisisitiza.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ambayo yanafanyika Machi 8 mwaka huu mkoani Simuyi ni “Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania sasa nay a baadaye’’.
Katika kongamano hilo wanawake wamelitumia kuonesha bidhaa mbalimbali wanazotengeza na kuzalisha katika Mkoa wa Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 19,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.