Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo yenye thamani ya shilingi bilioni nane.
Katika ziara aliyoifanya Novemba 29 mwaka huu,Kanali Thomas amekagua mradi wa miundombinu ya hospitali ya wilaya ya Namtumbo ambapo Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa alipofanya ziara alitoa maagizo ya kurekebisha milango yote 138 iliyopo katika hospitali hiyo ambapo hadi sasa milango 46 imerekebishwa.
Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Chiriku Chilumba kuhakikisha inapofika Desemba 10 mwaka huu kazi zote za umaliziaji ziwe zimekamilika ikiwemo ya kufunga milango yote katika hospitali hiyo .
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza ujenzi wa hospitali kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo amesema katika mwaka 2019/2020 serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo ya maabara,mionzi,wodi ya wanaume,wodi ya wazazi na upasuaji,
Kulingana na Mkurugenzi huyo mwaka 2020/2021,serikali ilileta fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji,ujenzi wa njia za kupita wagonjwa na ujenzi wa wodi ya Watoto.
Amesema mwaka 2020/2021 serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya jengo la upasuaji wanawake,jengo la bima,nyumba ya maiti na ukamilishaji wa wodi ya Watoto.
Hata hivyo amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imepokea kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya uendelezaji wa jengo la upasuaji katika wodi ya wanaume,wanawake na nyumba ya maiti.
Akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amekagua mradi wa ujenzi wa shule ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma inayojengwa eneo la Migelegele ambapo serikali kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza mradi huo.
Majengo yanajengwa katika shule hiyo inayotarajia kuanza kuchukua wanafunzi mwakani ni Pamoja na na jengo la utawala, madarasa vyumba 12,mabweni Matano, maabara tatu,vyoo,nyumba za walimu,ukumbi wa shule na bwalo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameipongeza Kamati ya ujenzi wa shule hiyo kwa kusimamia vema mradi huo ambapo amesema kila anapotembelea kukagua mradi kumekuwa na mabadiliko makubwa.
Katika ziara hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo,Mkuu wa Mkoa pia amekagua ujenzi wa daraja la Libango lenye urefu wa meta 30 ambapo serikali imetoa shilingi milioni 900 kutekeleza mradi huo.
Juma Kilaza mkazi wa Libango amesema wanaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambapo awali walikuwa wanapita kwenye kivuko cha miti na kwamba sasa mazao yanayolimwa kwa wingi katika Kijiji cha Libango yatasafirishwa kwa urahisi Kwenda Namtumbo.
Miradi mingine iliyokaguliwa na Mkuu wa Mkoa ni ukarabati na ujenzi wa barabara za vumbi la lami za Namtumbo mjini zenye urefu wa kilometa 30 na ujenzi wa kalaveti vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 970.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Novemba 29,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.