NAIBU Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewahakikishia wakazi wa wilaya ya Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma kuwa, Serikali imedhamiria kujenga barabara ya Mtwara Pachani-Lusewa- Nalasi kwa kiwango cha lami.
Kasekenya ametoa ahadi hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lusewa wilaya ya Namtumbo na Nalasi wilaya ya Tunduru mara baada ya kukagua barabara hiyo yenye urefu wa km 300, ambayo imeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Ruvuma na kusababisha adha kubwa kwa wananchi.
Alisema, dhamira ya Serikali ni kujenga barabara hiyo na barabara nyingine za katika mkoa wa Ruvuma ikiwamo ya Kitai-Lituhi-Mbambabay,Likuyufusi-Mkenda na Londo kwenda mkoa jirani wa Mororogoro.
Alisema, Serikali kupitia wizara ya ujenzi na uchukuzi iko katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa barabara hiyo ili kuunganisha mawasiliano kwa wakazi wa vijiji vya Namtumbo na Tunduru ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwa Makamu wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Alisema, barabara ya Mtwarapachani-Lusewa-Naalsi ni muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Ruvuma ambao ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara kama korosho ambalo linachangia pato na uchumi wa Taifa.
Alisema,barabara hiyo imeshafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina na wakala wa barabara(Tanroads) na kilichobaki ni Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi wake ambapo itakapokamilika itawaondolea wananchi kero ya usafiri waliokuwa wanaipata.
“lengo la Serikali ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inaunganisha vijiji vyote kwa barabara za lami kupitia wakala wa barabara za mjini na vijijini Tarura na Tanroads, na kwa barabara hii tayari tumeshafanya upembuzi na usanifu wa kina”alisena Naibu Waziri.
Aidha alisema, wakati wanaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami, kwa sasa wataanza kujenga madaraja na sehemu zote korofi ili iweze kupitika kwa urahisi na wananchi waendelea kutumia barabara katika shughuli zao za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Kasekenya,barabara ya Mtwara Pachani-Nalasi ni muhimu sio kiuchumi tu bali hata kwa ulinzi wa mipaka yetu, kutokana na mkoa wa Ruvuma kupatakana na nchi jirani ya Msumbuji ambayo katika siku za karibuni kumekuwa na tatizo kubwa la kiusalama.
Kasekenya amewaomba wananchi ,kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuinua hali zao za maisha na kuharakisha uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa alisema, barabara hiyo inategemewa na vijiji 36 vya wilaya ya Namtumbo na Tunduru na ndiyo uti wa uchumi kwa wilaya hizo kutokana na wananchi wake kuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula.
Aidha alisema kuwa,licha ya kutegemewa kiuchumi pia ni muhimu kiafya kwa sababu wananchi wengi pindi wanapougua wanaitumia barabara hiyo kwenda Hospitali ya wilaya Namtumbo umbali wa km 130 na Hospitali ya rufaa Songea kwenda kupata matibabu kwa kuwa hakuna barabara nyingine mbadala.
Ameiomba Serikali,wakati inasubiri kupata fedha kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami basi kufanya marekebisho maeneo korofi kwa kuweka lami nyepesi ili iweze kupitika kwa urahisi na wananchi waweze kuendelea kuitumia barabara hiyo katika shughuli zao za maendeleo.
Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa kutokana na kuwa na mipango mingi ya maendeleo iliyowezesha kumaliza baadhi ya kero na kukua kwa uchumi wa wananchi wa jimbo hilo.
Alisema, tatizo kubwa hasa katika mikoa ya Kusini ni kutokuwa na wawakilishi makini na wazuri wanaofahamu matatizo ya wapiga kura wao na wenye dhamira ya kweli katika kuwatumikia na kuwajali wananchi kama ilivyo kwa Mbunge wa Namtumbo Vita Kawawa.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.