Na Albano Midelo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema ndani ya siku saba kuanzia Mei 15,2024,serikali itatoa maamuzi ya uwepo wa soko moja au masoko matatu ya madini ya vito wilayani Tunduru.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea,Kanali Abbas amesema akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Tunduru hivi karibuni aliweza kutembelea masoko ya madini ya vito ambayo ni soko la Generation,TUDECU na kukagua ujenzi wa soko jipya la madini.
Amesema akiwa katika masoko ya madini ya Generation na TUDECU walijitokeza wananchi wengi ambao walitaka kupata ufafanuzi wa baadhi ya kero zinazowasumbua ambapo baadhi ya wananchi walijitambulisha kuwa ni wafanya biashara wa madini ya vito wilayani Tunduru.
Amesema wafanyabiashara hao waliiomba serikali kuwatafutia fursa za mikopo kwenye Taasisi za fedha ili waweze kufanya biashara za madini kwa ufanisi mkubwa.
Ameongeza kuwa wafanyabiashara hao pia walikuwa na hoja ya kutaka majibu ya serikali ni juu ya uwepo wa masoko Zaidi ya moja ya uuzaji wa madini ya vito wilayani humo.
“Kwa ugeni wangu niliona masuala haya hayahitaji majibu ya haraka,niliwashauri wanipe muda ili niweze kuwapatia majibu,leo nimewaita wanahabari kuwajulisha kwamba,jambo hilo serikali inalifanyia kazi kwa kuwa ni jambo linalohitaji utafiti mkubwa na majibu mazuri’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa amesema aliamua kuunda Tume maalum ya wataalam ambayo itakwenda kufanya utafiti wa hoja zote hizo ili majibu yatakayorudi yaweze kutoa maamuzi ya serikali juu ya uwepo wa soko moja au masoko matatu ya madini wilayani Tunduru.
Amesisitiza kuwa msimamo wa serikali utatolewa baada ya timu hiyo maalum kukamilisha kazi yake na kuleta majibu ndani ya siku saba.
Wilaya ya Tunduru ina utajiri wa karibu aina zote za madini ya vito isipokuwa madini ya tanzanite ambayo katika dunia nzima yanapatikana Mirerani mkoani Manyara.
Madini mengine yenye thamani kubwa aina ya shaba yamegundulika katika Kata ya Mbesa Tarafa ya Nalasi wilayani Tunduru.
Kugundulika kwa madini hayo kunaifanya wilaya ya Tunduru kuwa ndiyo wilaya pekee nchini na Afrika Mashariki na Kati kuwa na madini ya shaba mbalimbali zikiwemo kijani,bluu na njano.
Utafiti unaonesha kuwa Tarafa nzima ya Nalasi ina utajiri wa madini hayo ambayo yanaweza kuchangia kuinua uchumi wa wilaya hiyo,Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla wake.
Utafiti wa awali umebaini madini hayo yameenea hadi mto Ruvuma mpakani na nchi jirani ya Msumbiji na pia madini hayo yamesambaa hadi mpakani na wilaya ya Namtumbo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.