SERIKALI imeiagiza Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Sitakabadhi za Ghala kuhakikisha inaongeza idadi ya mazao yanayonunuliwa kupitia mfumo huo kutokana na kuwepo manufaa makubwa kwa mkulima na Taifa kwa ujumla.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigaghe(MB) wakati anazindua na kufunga mafunzo ya siku tatu kwa Waendesha Ghala kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha SAUT Tawi la Mtwara.
Amesema licha ya kuwepo changamoto chache katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za Ghala hapa nchini,serikali inatambua manufaa makubwa ya mfumo huo ambayo ameyataja kuwa ni mkulima kupata ulinzi sokoni na kunufaika na uzalishaji wake kwa kupata bei stahiki sokoni.
“Mfumo huu umekuwa kichocheo cha ukuzaji wa ajira rasmi na ajira zisizo rasmi hususan katika maeneo ya vijijini,mfumo umeleta tija ndiyo maana serikali imetoa agizo kwa Bodi kuhakikisha kuwa inaeneza mfumo huu kwenye mazao karibu yote katika nchi hii yakiwemo mazao ya chai,pamba,tumbaku na bidhaa nyingine ambazo sio za kilimo ili mradi ziwe na tija kupitia mfumo huu’’,alisisitiza Mhe.Kigaghe.
Ameyataja mafanikio mengine ya mfumo huo kuwa ni ongezeko la bei za mazao ambapo mapato ya Mkulima na serikali yameongezeka kwa wastani wa asilimia 200,ongezeko la uzalishaji wa mazao umeongezeka kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka na upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala.
Amesema mfumo huo pia umeongeza mapato ya uhakika kwa serikali Kuu na Serikali za Mitaa sanjari na kukuza huduma za fedha vijijini na kwamba mfumo unachochea ajira ambapo katika Kwa mujibu wa Naibu Waziri,msimu wa mwaka 2021/2022 kwenye zao la korosho pekee ghala 34 zilisajiriwa na kuwezesha kutoa ajira 1,258.
Hata hivyo amesema kati ya ajira hizo mfumo umetoa ajira rasmi 284 za wasimamizi wa Ghala na ajira zisizo rasmi 680 za wachukuzi mzigo,watoa huduma za chakula 340 na tripu za malori 23,000 za kupeleka na kutoa mzigo ghalani.
Akitoa taarifa mafunzo hayo,Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Usimamizi Stakabadhi za Ghala nchini Asangye Bangu amelitaja lengo ya mafunzo hayo kuwa ni kutoa elimu na kujenga uelewa wa Pamoja katika kutumia njia za kisasa na zenye tija katika usimamizi wa ghala unaowezesha uuzaji zao la korosho kabla ya msimu kuanza Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo amesema ghala zinajumuisha za watu binafsi serikali,Taasisi za Umma,ghala kuu za vyama vikuu vya ushirika na ghala za vyama vya msingi na mafunzo yatatua changamoto zilizopo kwenye mfumo ikiwemo masuala ya ubora wa mazao,upotevu wa mazao yakiwa ghalani na matumizi sahihi ya mizani.
Amezitaja mada ambazo zimefundishwa kwenye mafunzo hayo kuwa ni elimu ya mfumo wa stakabadhi Ghala,tathimini ya msimu wa korosho 2021/2022,matumizi ya vipimo vya unyevu ghalani na matumizi sahihi ya mizani ghalani.
Mada nyingine amezitaja kuwa ni matumizi ya mfumo wa usimamizi wa ghala kwa TEHAMA,miongozo ya usimamizi wa mazao ghalani,taratibu za kutunza kumbukumbu ghalani,sheria na kanuni zinazosimamia mfumo.
Mafunzo kwa waendesha Ghala yamekuwa yanatolewa kila mwaka kabla ya msimu wa zao la korosho kuanza ili Waendesha Ghala watambua sheria zinazosimamia utekelezaji wa mazao ya ghala.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Septemba 25,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.