Katika kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa bora na endelevu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, safari hii ikiwa ni kupitia mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Mbaha kilichopo katika Kata ya Mbaha, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia wakazi 7,851 wa vijiji vinne vyenye jumla ya vitongoji 30. Tayari Halmashauri imepokea kiasi cha Sh851 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao umeanza kutekelezwa na Kampuni ya Nakahegwa Engineering kutoka Songea, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo saba ya msingi, yakiwemo jengo la OPD, jengo la wazazi, maabara, upasuaji, kufulia, kichomea taka na nyumba ya watumishi.
Mhandisi Othman King wa Halmashauri ya Nyasa amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 20 na unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya huduma za afya kwa wananchi wa maeneo hayo. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Khalid Khalif amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa na kutoa wito kwa mkandarasi kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Dkt. John Damian Mrina amesema Wilaya ina hospitali moja, vituo vya afya vitano na zahanati 25 zinazohudumia jumla ya watu 191,193, hivyo ujenzi wa kituo hicho utapunguza presha kubwa ya upatikanaji wa huduma bora za afya katika eneo hilo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.