WADAU wa kilimo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,wameipongeza serikali kwa hatua iliyochukua ya kuanza kuelekeza fedha kwa ajili ya ukamilishwaji wa miradi ya kilimo ikiwemo ya ujenzi wa ghala la kuhifadhia nafaka katika kata ya Magagura wilayani humo ambayo ilifanyiwa ufuatiliaji na asasi ya millenium Arts group na kuonekana kuwa na changamoto ya kushindwa kukamilika kwa muda mrefu na kutoa tija kwa wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni na Afisa pembejeo wa Halmashauri hiyo Ephraim Nyakunga wakati alipokuwa akichangia hoja katika mafunzo ya utawala Bora na ufuatiliaji wa rasilimali za umma(PETS)yaliyoandaliwa na asasi hiyo kupitia ufadhili wa The Foundation For Civil Society.
Nyakunga alisema kuwa tangu asasi hiyo ianze kutekeleza mradi wa utawala Bora na ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika kata nane za Halmashauri hiyo matokeo chanya yameanza kuonekana ikiwa pamoja na serikali kuchukua hatua ya kuelekeza fedha kwa ajili ya ukamilishwaji wa mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia nafaka katika kata ya Magagura wilayani humo.
Aidha alisema kuwa Halmashauri hiyo pia imeweza kufanya maboresho kwenye baadhi ya maeneo ambayo yalionekana kuwa na changamoto wakati wa ugawaji wa pembejeo za Ruzuku za kwa msimu uliopita baada ya asasi hiyo kufanya ufuatiliaji kwenye miradi ya sekta ya kilimo wilayani humo.
Awali kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo John Mosha akifungua mafunzo hayo ameipongeza asasi hiyo ya Millenium Arts Group kwa kuchochea kasi ya maendeleo ambapo ameiagiza Idara ya mipango na kilimo kuendelea kutoa ushirikiano kwa asasi hiyo.
Akizungumza katika mafunzo hayo mkurugenzi mtendaji wa asasi hiyo Mnung’a Shaib Mnung’a alisema kuwa mradi huo wa utawala Bora unatekelezwa katika kata nane za Magagura,Kizuka,Mpitimbi,Litapwasi,Peramiho,Litisha,Muhukuru na Lilahi kwa kipindi cha miezi nane kwa gharama ya shilingi milioni 42 za kitanzania lengo likiwa ni kupata matokeo chanya katika miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake mshauri mwelekezi katika masuala ya utawala Bora Lawrence Chuma alisema kuwa changamoto kubwa inayojitokeza kwa Nchi nzima ni kukosekana kwa uwajibikaji,uwazi na ushirikishwaji kati ya viongozi na wananchi katika shughuli za maendeleo.
Imeandikwa na Julius Konala
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.