Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga kiasi cha shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uhasibu Kampasi ya Songea.
Mradi mkubwa wa elimu ya juu unatarajiwa kubadilisha taswira ya Mkoa wa Ruvuma kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi lililopo katika eneo la Pambazuko Manispaa ya Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema ujenzi wa majengo ya awamu ya kwanza unatarajiwa kuanza mara moja ukitekelezwa na kampuni ya China Aero Technology kutoka China.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema serikali imeweka mkazo mkubwa kuhakikisha chuo hicho kinajengwa kwa viwango vya ubora wa kimataifa, ili kizazi cha sasa na vijavyo kinufaike na uwekezaji huo mkubwa.
“Ni matumaini yangu kuwa ujenzi huu utasimamiwa ipasavyo kwa ajili ya kuhakikisha fedha za Serikali zinazotumika zinalenga kupata chuo chenye miundombinu imara, bora na endelevu,” alisema Kanali Ahmed huku akisisitiza dhamira ya Serikali kuimarisha elimu ya juu nchini.
Kanali Ahmed ametumia nafasi hiyo pia kutoa rai kwa uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kuhakikisha wakazi wa Ruvuma wanapewa kipaumbele katika nafasi mbalimbali za ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo.
“Tunaamini ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zitatolewa, hivyo tunaleta ombi rasmi kwa uongozi wa chuo na mkandarasi kuhakikisha fursa hizi zinawanufaisha wananchi wetu,” alieleza kwa msisitizo RC Abbas.
Katika kuunga mkono jitihada za kukuza uchumi wa ndani, Mkuu wa Mkoa amehimiza matumizi ya malighafi na huduma zinazopatikana ndani ya mkoa huo ili kuchochea biashara na kuinua kipato cha wakazi wa Songea na maeneo jirani.
Ametaja bidhaa kama mbao, mchanga, kokoto na vyakula kuwa ni miongoni mwa mahitaji yanayoweza kupatikana kutoka kwa wazalishaji wa ndani na kusaidia kupanua wigo wa ushiriki wa jamii.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,kwa kutoa fedha za ujenzi wa chuo hicho kikuu, huku akiahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iko tayari kushughulikia changamoto zote zitakazojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha Profesa Eliamani Sedoyeka amesema Chuo hicho kipya kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 10,000 wa programu mbalimbali, jambo linaloashiria mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu na uchumi wa mkoa wa Ruvuma.
Amesisitiza kuwa Chuo Kikuu hicho kitakuwa ni miongoni mwa vyuo vikuu vikubwa hapa nchini na fursa kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na ukanda wa kusini kwa ujumla.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.