SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 1.4 kujenga shule mpya tatu za sekondari katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa shule hizo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas,Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Dkt.Julius Lingu amezitaja shule hizo kuwa ni Nakayaya,Majimaji na Lumbukule.
Amesema shule hizo zinajengwa kupitia Programu ya Uboreshaji Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) ambapo kila shule imepewa shilingi milioni 470 kutekeleza mradi huo.
“Ujenzi wa shule hizo bado unaendelea,kuna mapungufu ambayo yamejitokeza katika ukaguzi uliofanywa na Mkuu wa Mkoa hivyo mapungufu hayo yatafanyiwa kazi na kufanyiwa marekebisho ili shule hizo ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ifikapo Januari 2023’’,alisisitiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru Chiza Marando ameyataja majengo yanayojengwa katika kila shule kuwa ni ujenzi wa maabara tatu,vyumba nane vya madarasa,matundu 20 ya vyoo,jengo la utawala,minara miwili ya maji,jengo la TEHAMA na jengo la maktaba.
Akizungumza mara baada ya kukagua shule hizo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 7.7 kutekeleza ujenzi wa shule mpya 11 za sekondari mkoani Ruvuma.
Kati ya shule hizo mpya, shule tatu zinajengwa katika wilaya ya Tunduru hivyo RC Thomas amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kusimamia ujenzi wa shule hizo na kuweka samani zake katika kila darasa ili shule hizo zianze kuchukua wanafunzi Januari 2023.
“Mhe.Rais alishamaliza kazi yake ya kututafutia pesa kutuletea hivyo ni wajibu wetu sisi sote kama timu kusimamia na kuhakikisha miradi ya serikali inatekelezwa kwa viwango na thamani inayolingana na fedha’’,alisisitiza.
Serikali Kuu kupitia Programu ya Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) inajenga shule mpya za sekondari 1000 katika nchi nzima,kati ya hizo shule 11 zinajengwa katika Mkoa wa Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 5,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.