SERIKALI ya awamu ya tano imetoa zaidi ya shilingi bilioni 16 kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mkoani Ruvuma hali iliyoweza wananchi 1,149,867 kupata maji safi na salama hadi kufikia mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika Mkoa wa Ruvuma hivi sasa ni asilimia 63.9 ya wakazi wote wa Mkoa idadi ambayo imeongezeka kutoka asilimia 57 ya wananchi waliokuwa wakipata huduma hiyo mwaka 2015.
Hata hivyo Mndeme amewataja wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama wanakadiriwa kuwa 888,005 ambao ni sawa na asilimia 61.6,ambao wanapata maji kupitia vituo vya kuchotea maji 5,631.
“Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama na kufikia malengo ya kitaifa, Mhe, Rais ameendelea kuwezesha ukarabati na ujenzi wa miradi mipya ya maji, kuanzisha na kusajili kisheria jumuiya za watumia maji vijijini kwa ajili ya kusimamia na kuendesha miradi ya maji’’,alisema.
Kuhusu huduma ya maji mijini,Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa wa Ruvuma una miji sita ambayo ni makao makuu ya Halmashauri ukiwepo mji wa Songea ambao ni makao makuu ya Mkoa. Miji hiyo ni Songea, Mbinga, Tunduru, Namtumbo, Mbambabay na Madaba.
Mndeme amesema Hadi kufikia mwaka 2020 hupatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Manispaa ya Songea umefikia asilimia 91 ikilinganishwa na asilimia 72.7 kwa mwaka 2015.
Ameutaja Mpango wa utekelezaji miradi ya maji vijijini katika mwaka wa fedha 2019/2020,serikali imeupatia Mkoa wa Ruvuma kiasi cha shilingi 1,168,888,500.83 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miradi 29 ya maji.
Mndeme amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020,serikali imeupatia Mkoa wa Ruvuma shilingi bilioni 7.8 kwa ajili ya Kujenga, kukarabati na kufanya upanuzi katika miradi 33 ya maji katika wilaya zote tano .
Akizungumzia hali ya utekelezaji wa miradi kupitia programu ya lipa kwa matokeo na Mfuko wa Maji,Mkuu wa Mkoa amesema hadi kufikia mwaka 2020 Kupitia Program ya lipa kwa matokeo , Jumla ya miradi 19 imekamilika,miradi kumi inaendelea kutekelezwa na miradi 33 iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Ameongeza kuwa katika kukabiliana na tatizo la maji, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya maji na kupanua mitandao ya maji ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Maelekezo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ni kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama vijijini unaongezeka toka asilimia 67.7 mwaka 2015 na kufikia asilimia 85 mwaka 2020; miji ya makao makuu ya Mikoa toka asilimia 68 mwaka 2015 na kufikia asilimia 95 mwaka 2020 na miji mikuu ya Wilaya na miji midogo toka asilimia 57 mwaka 2015 hadi asilimia 90 mwaka 2020.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 29,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.