Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, inatarajia kuanza ujenzi wa Kituo cha afya katika Kata ya Kingerikiti, tarafa ya Mpepo, Kwa Lengo la kutatua kero ya wananchi wa kata hiyo waliokuwa wakisafiri umbari mrefu wa takriban Kilometa arobaini (40), kufuata huduma za matibabu katika Wilaya ya Mbinga.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Bw. Jimson Mhagama, jana wakati akiongea na wananchi wa Kata ya Kingerikiti kwa lengo la kutambulisha mradi na kuwashirikisha Wananchi ili waweze kushirikiana na Serikali kwa lengo la kutekeleza Mradi huo.
Mhagama alifafanua kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imepokea Shilingi milioni mia mbili tu (Tsh 200,000,000/=) toka Serikali kuu kwa lengo la kujenga kituo cha afya cha Kingerikiti, ili kuwaletea huduma karibu za matibabu kwa wananchi wa kata hiyo, hivyo kwanza kabisa wananchi mnatakiwa kufahamu mradi huu na kushirikiana na Serikali kuhakikisha ujenzi huu unakamilika ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.
Mhagama aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya Afya katika Wilaya ya Nyasa kwa kuhakikisha inatatua matatizo ya wananchi, hususani kwenye sekta ya afya, kwa kushirikiana na wananchi wa sehemu husika kwa kuangalia jiografia ya Wilaya.
Kwa upande wao Wananchi wa Kata ya Kingerikiti walimpongeza Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli, na Mh. Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya ambaye ni Naibu waziri wa Viwanda na Biashara kwa kutekeleza ahadi yake kwa kuwa aliahidi na ametekeleza ahadi yake ya kuwajengea Kituo cha afya cha Kingerikiti.
“Sisi wananchi wa Kata ya Kingerikiti, tumeupokea mradi huu na tunampongeza sana Mbunge wetu na Mh, Rais John Magufuli kwa kutujengea Kituo cha afya katika kata yetu kwa kuwa tulikuwa tunatembea umbali mrefu wa takribani kilometa 40 kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Litembo iliyoko wilayani Mbinga au Hospitali ya Wilaya ya Mbinga, hivyo tupewe majukumu yetu na tutahamasishana ili Ujenzi huu utekelezwe kwa muda uliopangwa.” alisema Wiligs ndunguru mkazi wa kijiji cha Kingerikiti kwa niaba ya wananchi wote.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Nyasa Dkt Aaron Hyera, aliwaambia wananchi kuwa mara baada ya kukamilika kwa kituo hicho cha afya cha kingerikiti kwa jiografia ya Wilaya ya Nyasa, huduma za afya zitatolewa vizuri kwa kuwa wagonjwa watakuwa hawatembei umbali mrefu na kupata huduma kwa wakati. Aliwataka wananchi hao kushiriki kikamilifu kujenga kituo hicho cha afya ambacho kipo katika Tarafa ya Mpepo na kwa sasa Tarafa ya Mpepo itakuwa na Vituo viwili vya Afya vya Serikali ambavyo ni Liparamba na Kingerikiti.
Aidha uboreshajiwa sekta ya afya katika Wilaya ya Nyasa umeimarika kwa kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, iliyojengwa Kijiji cha Nangombo Kata ya Kilosa Tarafa ya Ruhekei na Vituo vya Afya Kihagara,Mbambabay na Mkili vitafanya idadi ya Vituo Vya Afya kuwa Vitano (05) kitakapokamilika kituo cha Afya cha Kingerikiti.
Imeandaliwa
Na Netho C. Sichali
Kaimu Afisa habari (W) Nyasa
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.