SERIKALI ya Awamu ya Tano imetoa shilingi milioni 798 kwa ajili ya kukarabati sekondari kongwe ya wavulana Tunduru mkoani Ruvuma yenye wanafunzi zaidi ya 700 ambayo ilianzishwa mwaka 1978.
Mkuu wa shule hiyo Limia Ausi amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu imetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kukarabati madarasa,mabweni,ujenzi wa choo kipya,banda la mlinzi na kwamba nyumba za walimu haziusiki katika ukarabati huo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo,ukarabati umeanza Agosti mwaka huu na kwamba ukarabati unafanyika huku ratiba ya masomo kwa wanafunzi inaendelea kama kawaida hali ambayo imefanya kazi ya ukarabati kufanyika polepole bila kuathiri masomo ya wanafunzi.
“Inatulazimu wanafunzi kuwahamisha katika baadhi ya madarasa na wakati madarasa yao yanaendelea kukarabatiwa,ujenzi hivi sasa umefikia zaidi ya asilimia 90,tunafanya ukarabati kwa njia ya force akaunti’’,alisema Ausi.
Amesema ukarabati upo katika hatua za mwisho na kwamba tayari umefanyika kwenye jengo la utawala,kwenye vyumba vya madarasa 16,mabweni sita ambapo amesema shule hiyo ilijengwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1978 kwa ajili ya watoto wa wakimbizi wakati wa harakati za ukombozi katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika.
Hata hivyo amesema baada ya harakati za ukombozi kukamilika umoja wa mataifa waliikabidhi shule hiyo serikalini ambapo serikali ilianza kuwachukuwa wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali nchini na kuwapeleka Tunduru kwa ajili ya elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Wanafunzi wa kwanza walimaliza kidato cha nne mwaka 1982,hivi sasa sekondari ya Tunduru inachukuwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita pekee ambapo tunatoa combination saba zikiwemo PCM,PCB,PGM,CBG,HGL na HKL’’,alisema Ausi.
Amesema kutokana na shule hiyo kujengwa kwa ajili ya harakati za ukombozi,ili kuwaenzi mashujaa wa harakati hizo,shule hiyo imetoa majina ya viongozi mbalimbali wa Afrika kwenye mabweni vile MWL.Nyerere,Samaro Machel,Keneth Kaunda,Robeth Mgabe, Netho,Nkurumah na Mandela.
Mkuu huyo wa shule kwa niaba ya walimu ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za ukarabati wa shule hiyo ambayo ilikuwa na majengo chakavu ambayo yalikuwa kero kwa wanafunzi na walimu.
Abdalanus Sala mwanafunzi wa kidato cha sita katika sekondari ya Tunduru ameishukuru serikali kwa kumaliza kero ya mazingira magumu ya miundombinu ya madarasa,vyoo na mabweni ambapo amesema wanafunzi hivi sasa wanasoma kwenye mazingira bora ya kufundishia.
Robson Gatson Mwanafunzi Tunduru Sekondari amepongeza mpango wa serikali kukarabati sekondari kongwe nchini ambapo amesema mwanafunzi amejengewa mazingira mazuri ya kusomea mchana na usiku hali ambayo itaongeza ufaulu katika mitihani yake ya mwisho.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Desemba 9,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.