MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewapongeza Wakala wa Barabara TANROADS mkoani Ruvuma kwa kufanya kazi ya ziada ya kukabiliana na maafa katika miundombinu ya madaraja na barabara unaotokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika mkoa mzima.
Mndeme ametoa pongezi hizo baada ya kukagua daraja la Lukumbo katika Kata ya Mtipwili wilayani Nyasa ambalo limekatika na kusababisha kero ya usaifiri na usafirishaji kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo ambayo inakwenda hadi mpakani mwa nchi ya Msumbiji.
“TANROADS Ruvuma mnafanyakazi kubwa sana kwa sababu athari zinazoletwa na mvua katika Mkoa wetu ni kubwa sana,leo tupo Nyasa katika Daraja la Lukumbo,lakini hivi tunavyoongea TANROADS wapo Lukumbule Tunduru wanarudisha mawasiliano,TANROADS wapo Nalasi,wapo mawe ya bunduki,wapo Madaba,wapo daraja la Mnyamwaji wanarudisha mawasiliano,suala la athari za mvua hakuna wa kumnyoshea kidole’’,alisisitiza Mndeme.
Amesema TANROADS hivi sasa usiku na mchana wapo kazini ambapo amewapongeza kwa hatua ya haraka ya kurudisha mawasiliano katika daraja la Lukumbo ambapo ametoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi cha mvua nyingi hasa wanapopita katika madaraja,makalavati na kwenye mito.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya licha ya kutoa pongezi kwa serikali kwa kuanza matengenezo ya daraja hilo ambalo lipo katika Jimbo lake,amesema barabara nyingi jimboni humo hivi sasa zimeharibika kutokana na mvua zinazoendelea .
Hata hivyo amesema TANROADS imejipanga vizuri katika matengenezo ya barabara hizo na kwamba fedha kwa ajili ya marekebisho na matengenezo zimetengwa.
Kutokana na umuhimu wa barabara hiyo ambayo ipo mpakani na nchi ya Msumbiji,Mhandisi Manyanya ametoa rai kwa serikali kupitia TANROADS itengwe bajeti ya kutosha ili kujenga daraja bora kati ya mawili yaliyoharibika katika eneo hilo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 3,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.