WAKALA wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,imeanza kujenga barabara za lami za mitaa katika mji wa Namtumbo ikiwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya sita ya kuwavutia wawekezaji kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali ardhi na misitu.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023,serikali kuu imeipatia Wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)Sh.milioni 890 kwa ajili ya kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 1.6 katika mji wa Namtumbo.
Aidha fedha hizo,zimetumika kufunga taa za barabarani zinazotumia umeme wa jua na kujenga mitaro ya kupitishia maji ya mvua kwenda katika maeneo husika ambayo awali yalilazimika kwenda kwenye makazi ya wananchi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wilayani humo Mhandisi Fabian Lugalaba,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara za mitaa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Namtumbo.
Alisema,lengo kuu la kujenga barabara hiyo ni kuwawezesha wananchi wa mji wa Namtumbo kuwa na mawasiliano ya uhakika kutoka kwenye maeneo yao kwenda makao makuu ya wilaya zilipo ofisi ya Mkuu wa wilaya,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na maeneo mengine ya huduma za kijamii.
Alisema,TARURA imeamua kujenga na kuimarisha miundombinu ya barabara katika mji huo ili kuiwezesha serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kuibua fursa za uwekezaji na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya ya Namtumbo na mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wake,kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo mji wa Namtumbo ulikuwa na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 0.9 tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa miaka 14 iliyopita,hivyo kuongezeka kwa barabara ya Namtumbo-shule imesaidia sana kurudisha hadhi ya mji huo.
Ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuiongezea TARURA fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya barabara na kuhaidi kuwa,fedha zote zilizopelekwa zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuchochea kukua kwa uchumi na maisha ya wananchi.
Lugalaba,amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza barabara hizo zinazojengwa katika maeneo yao kwa kutozidisha uzito,kutomwaga mafuta,kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo kando kando ya barabara ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Wakazi wa Namtumbo,wameipongeza serikali kupitia Tarura kujenga barabara hiyo ambayo imesaidia sana kuupundezesha mji huo na kuwawezesha kufanya shughuli zao za kujipatia kipato kwa masaa 24 tofauti na hapo awali.
Joseph Hokororo alisema,kabla ya barabara hiyo kujengwa kwa lami wakati wa masika kero kubwa ilikuwa matope mengi na hata majira ya kiangazi kulikuwa na vumbi kubwa lililoingia ndani ya nyumba na hivyo kuathiri sana afya zao.
Aliongeza kuwa,kujengwa kwa kiwango cha lami barabara hiyo kumesaidia maeneo yao kuwa na hadhi kubwa na hivyo kushawishi watu wengi kuhitaji maeneo kwa ajili ya makazi na shughuli nyingine za kiuchumi.
Hilal Mgawe alisema,uwepo wa mradi huo umesaidia sana vijana kupata ajira za muda na hivyo kupata fedha za kujikimu ambapo ameiomba serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itakwenda kuinua hali zao za maisha.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.