MKOA wa Ruvuma una Jumla ya kilometa 4,130.63 za mtandao wa Barabara zinazosimamiwa na TARURA ambazo hupitika kwa mwaka mzima.
Kwa Mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Wahabu Nyamzungu barabara hizo zipo katika hali nzuri kwa wastani wa asilimia 57.80.
Hata hivyo Nyamzungu amesema kilometa 3,015.59 za mtandao wa Barabara zilizosalia sawa na asilimia 42.20 hupitika kikamilifu wakati wa kiangazi tu.
Amesema Serikali kupitia TARURA inaendelea na juhudi ili kuufanya mtandao wote wa Barabara kupitika kwa misimu yote ya Mwaka mkoani Ruvuma.
“Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia TARURA Mkoa wa Ruvuma ulitengewa zaidi ya shilingi bilioni 24, katika bajeti hiyo, TARURA iliingia mikataba 75 na Wakandarasi ili kuufanya mtandao wa barabara kupitika mwaka mzima’’,alisisitiza.
Mhandisi Nyamzungu amesema katika mikataba hiyo zaidi ya shilingi bilioni 19 zilitengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali za matengenezo ya barabara, ujenzi wa madaraja pamoja na makalavati.
Hata hivyo amesema Hadi kufikia Juni,2022 mikataba 70 ya Mfuko wa fedha za Barabara, Jimbo na Tozo ilikamilika kwa asilimia 100 ambapo mikataba mitano ilivuka mwaka na ipo katika hatua za mwisho za umaliziaji.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za mapato ya ndani kwa ushuru na maegesho katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023,Mhandisi Nyamzungu amesema, yamefanyika maboresho ya barabara ya Mjimwema Halmashauri ya Mji wa Mbinga yenye urefu wa kilometa 1.1 kwa kiwango cha lami iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 497.
Ameongeza kuwa TARURA Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka huu wa fedha inatekeleza miradi 16 ya maendeleo inayogharimu zaidi ya shilingi bilioni 14 na kwamba miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Hata hivyo amesema kati ya miradi hiyo kupitia Fedha za Mfuko wa Jimbo inatekelezwa Miradi mitano na kupitia tozo inatekelezwa miradi 11.
Amesema Serikali Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia TARURA Mkoa wa Ruvuma imetoa shilingi milioni 750 kwa lengo la kufanya Matengenezo ya barabara ya Luhindo-Mpepo hadi Darpori katika Halmashauri ya Nyasa.
Amesema matengenezo hayo yanahusisha Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha Changarawe na madaraja na kwamba hatua za utekelezaji wa mradi huo zipo katika hatua za umaliziaji.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.