Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Ruvuma umeidhinishiwa jumla ya Shilingi Bilioni 38.29 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Silivester Chinengo anasema fedha hizo zinatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji, kuboresha maisha ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia miundombinu bora ya barabara.
Ufadhili wa Miradi na Matumizi Yake
Kati ya kiasi hicho cha fedha kilichoidhinishwa, Shilingi Bilioni 22.19 zinatoka katika Mfuko wa Barabara (Road Fund), Mfuko wa Jimbo pamoja na Tozo ya Mafuta.
Kulingana na Meneja huyo wa TARURA Mkoa,fedha hizo zitatumika kujenga na kukarabati jumla ya kilometa 1,264.68 za barabara, ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na Kilometa 6.85 za barabara za lami,Kilometa 398.86 za barabara za changarawe,Kilometa 858.97 za uchongaji barabara,Ujenzi wa madaraja 49,Ujenzi wa makaravati 57 na Ujenzi wa mitaro yenye urefu wa mita 2,610
Mbali na fedha hizi, TARURA Ruvuma pia imepokea Shilingi Bilioni 16.20 kutoka kwa wafadhili wa Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Agri-Connect.
Fedha hizo zinatumika kujenga barabara ya Utiri – Mahande yenye urefu wa kilometa 14.41 kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Mbinga. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara ili kusaidia sekta ya kilimo na uchukuzi wa mazao, jambo linalosaidia kuinua uchumi wa wakazi wa eneo hilo.
Faida za Uboreshaji wa Barabara
Utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wakazi wa Ruvuma. Barabara bora zitapunguza gharama za usafiri, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na mazao ya kilimo, na pia kuchochea maendeleo ya biashara katika maeneo mbalimbali.
Aidha, ujenzi wa madaraja na makaravati utawezesha wananchi kusafiri kwa urahisi hata wakati wa mvua kubwa, hivyo kuimarisha usalama wa barabara na usafirishaji.
TARURA Ruvuma imejipanga kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo katika kuboresha miundombinu ya barabara.
Kupitia uwekezaji huu mkubwa, wakazi wa Ruvuma wanatarajia kuona mabadiliko chanya katika sekta ya usafirishaji, hali itakayokuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.