WAKALA wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imepokea zaidi ya shilingi Bilioni nne kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wilayani Namtumbo Mhandisi Fabian Lugalaba,wakati akitoa taarifa ya hali ya matengenezo na maboresha miundombinu ya mtandao wa barabara na kueleza kuwa,fedha hizo zimewezesha kufungua mtandao wa barabara maeneo yasiyofikika kiurahisi na ujenzi wa madaraja.
Lugalaba alisema,kati ya fedha hizo shilingi bilioni 2.684 zilipokelewa na kutumika kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa km 133.62.
Kwa mujibu wa Lugalaba,barabara zenye urefu wa kilomita 103 zilikuwa ni matengenezo ya kawaida na kilomita 30 barabara kwa kiwango cha changarawe.
Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Tarura itatumia jumla ya shilingi bilioni 1.409 kufungua barabara mpya kilomita 24,kujenga barabara za lami kilomita 1.6 kufanya matengenezo kwa kiwango cha changarawe kilomita 10 kufanya ukarabati wa kawaida kilomita 161 na kujenga makalavati 4.
Lugalaba alitaja vyanzo vya fedha hizo ni kutoka mfuko wa matengenezo ya barabara,fedha za maendeleo kutoka mfuko wa barabara,fedha za nyongeza ya tozo kwenye mafuta na fedha kutoka mfuko mkuu wa serikali(jimbo).
Baadhi ya wananchi wilayani humo,wameipongeza serikali kwa kusimamia matengenezo ya barabara ambazo zimesaidia kuboresha na kurahisisha mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aden Nchimbi alisema,katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan serikali kupitia Tarura,imefanya kazi kubwa ya kufungua na kutengenezo barabara ambazo zimesukuma maendeleo na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wilaya ya Namtumbo.
Said Ngonyani mkazi wa Minazini wilayani humo,amewapongeza watumishi wote wa Tarura kwa matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na serikali na usimamizi makini wa miradi ya barabara katika maeneo mbalimbali ambao umesaidia kuifungua wilaya hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.