Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewapongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) mkoani Ruvuma kwa kufanya maboresho mbalimbali ya utoaji huduma kwa wateja.
Kanali Thomas ametoa pongezi hizo wakati anafungua kikao cha wadau wa TEMESA kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chandamali mjini Songea.
Amesema kwa muda mrefu wadau wa TEMESA walikuwa na malalamiko kadhaa kuhusu huduma zisizoridhisha ikiwemo gharama kubwa za matengenezo,matengenezo kuchukua muda mrefu,matengenezo kujirudia,upungufu wa watumishi,kuchakaa kwa miundombinu na uhaba wa vitendea kazi.
“Mtendaji Mkuu wa TEMESA ameyataja maboresho mbalimbali ambayo yanatarajia kufanywa ili kuboresha huduma ikiwemo kuingia mikataba na wazabuni wa vipuri na vilainishi ili kupunguza muda wa ununuzi’’,alisisitiza RC Thomas.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameipongeza serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kukarabati karakana na kununua vitendea kazi katika karakana ya TEMESA mkoani Ruvuma hali ambayo amesema itaongeza ufanisi katika kazi.
Amesisitiza kuwa mikakati na maboresho yanayoendelea yakisimamiwa vizuri huduma inayotolewa na TEMESA itakuwa bora na rafiki kwa wadau.
Awali Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TEMESA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda amesema Serikali imesaidia kufanya maboresho makubwa yanayoonekana katika Taasisi ya TEMESA.
Ameyataja baadhi ya maboresho yanayoendelea ni kukarabati ofisi za TEMESA katika mikoa ya Ruvuma,Mbeya,Arusha,Mwanza,Dodoma ,Tanga,Morogoro,Lindi,Mtwara,Mara,Kigoma,Tabora na Kagera.
Maboresho mengine ameyataja kuwa ni ununuzi wa vivuko vipya na kununua vitendea kazi hali ambayo imetatua changamoto kubwa zilizokuwa zinaikabili TEMESA na kwamba mwaka huu imetengwa bajeti ya zaidi ya shilingi 700 kwa ajili ya kununua vitendea kazi vya kisasa.
Naye Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TEMESA Josephine matiro amesema serikali imedhamiria kuboresha huduma zinazotolewa na TEMESA kwa lengo ya kutoa huduma bora na zenye viwango kwa wateja wao.
Amesema TEMESA ameamua kufanya vikao ya wadau wake kutoka mikoa yote 26 ili kupata maoni ya wadau inayowahudumia ili kutoa huduma zenye tija .
Mmoja wa wadau wakizungumza kwenye kikao hicho Wakili Julius Mtatiro ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ametoa rai kwa watendaji wa TEMESA nchini kuweka mikakati ya kuwafikia wadau wote badala ya kutegemea Taasisi za serikali.
Amesema watu binafsi sasa wanaweza Kwenda kutengeneza magari yao TEMESA baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa hivyo kuvutia wateja wengi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.