MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amefungua mafunzo ya Tume ya Ushindani FCC ambayo yametolewa kwa vijana 100 wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Mafunzo hayo yenye lengo la kujifunza misingi na sheria za ushindani katika shughuli za kibiashara na kumlinda mlaji ,yamefanyika katika hoteli ya St.Vinsent House Kilosa mjini Mbambabay yameshirikisha vijana kutoka Kata zote 20 zilizopo katika Halmashauri ya Nyasa.
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewataka vijana waliopata mafunzo hayo kwenda kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha wengine kwa ajili ya masilahi mapana ya uchumi endelevu wa Taifa.
Amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yataleta mfumo sawa wa ushindani ili kupata fursa sawa na kushauri elimu hiyo iwe sehemu ya maisha katika biashara na uchumi ili kusaidia kulinda viwanda vya ndani.
“Wilaya ya Nyasa ipo mpakani,naomba muwe makini na bidhaa bandia zisizokubalika kisheria katika nchi yetu,zinaweza kuingizwa nchini kinyemela na kuleta madhara au ushindani usio kuwa wa haki ikiwemo kutolipa kodi ya mapato’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme amezitaja bidhaa zenye changamoto za uingizaji kinyemela hapa nchini kuwa ni pamoja na sukari ambayo inaweza kuonekana inauzwa bei nafuu,ambapo ubora wake mara nyingi huwa ni hafifu.
Amesema ili kulinda mafuta yanayozalishwa na viwanda vya ndani,serikali iliongeza bei ya kodi kwa mafuta ya kula yanayoingizwa kutoka nje ya ya nchi ambapo mafuta ghafi hulipiwa kodi ya asilimia 25 na mafuta yaliyosafishwa hulipiwa kodi ya asilimia 25.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani FCC Joshua Msomi ameseme Tume hiyo inafanya kazi ya udhibiti bidhaa bandia kwa mujibu wa sheria ya alama za bidhaa ya mwaka 1963.
Ametayaja baadhi ya mambo yanayofanikisha kutambua bidhaa bandia kuwa ni ufungashaji wa bidhaa bandia huwa sio bora ukilinganisha na bidhaa halisi na rangi huwa hafifu.
“Mara nyingi bidhaa zinazolalamikiwa na mzalishaji asilia huwa hazitengenezwa na wazalishaji halisi ama moja kwa moja au kwa kibali maalum,huwa ni bandia’’,alisema Msomi.
Hata hivyo amesema bidhaa bandia zina athari kwa afya zinazohatarisha usalama wa mali na maisha na kwamba zinaongeza umasikini kwa kukulazimisha kununua mara kwa mara kutokana na kuharibika haraka.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 5,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.