WAKATI mchakato wa kumpata mwekezaji katika Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori Nalika wilaya yaTunduru mkoani Ruvuma ukitarajiwa kukamilika wiki ijayo,baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Rahaleo na Mbungulaji kata ya Kalulu wameiomba Bodi ya ushauri wa maliasili ya wilaya hiyo na Serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utalii kuchagua mwekezaji mwenye sifa atakayesaidia kukuza sekta ya utalii na kulipa kodi za Serikali na kushirikiana na jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wakiongozwa na Diwani wa kata ya Kalulu Mbale Motamota wamesema,wilaya ya Tunduru inazungukwa na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere pamoja na Jumuiya mbalimbali za Wanyamapori ikiwamo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Nalika ambayo katika kipindi cha miaka mitano imeongoza kutembelewa na idadi kubwa ya watalii wanaoingia katika wilaya hiyo.
Said Pachana mkazi wa Rahaleo alisema,kwa miaka mingi hawakuwa na mwekezaji,lakini ilipofika mwaka 2017 walipata mwekezaji mmoja kampuni ya Best Luxury Safaris ambaye aliwezesha utalii kukua japo kwa ugumu kutokana na hali mbaya ya miundombinu ya kitalu.
Alisema,mwekezaji huyo amefanya kazi nzuri ya kuwafikisha apa walipo na wanaamini kama wataendelea kushirikiana naye wanaweza kuwa mfano mzuri kwa wana Kusini na Tanzania kwa ujumla katika suala zima la uwekezaji katika sekta ya utalii.
Pachana,ameiomba bodi ya ushauri wa mambo ya maliasili ngazi ya wilaya,jumuiya ya Nalika na kamati ya mchakato wa kumpata mwekezaji kutowapa nafasi watu watakaorudisha nyuma juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuendeleza sekta hiyo hapa nchini.
Sharifu Galimbe mkazi wa Rahaleo, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa jitihada zake za kuboresha sekta hiyo,hata hivyo ameishauri kuwa makini na baadhi ya watu wanaoomba kuwekeza katika Jumuiya ya Wanyamapori ya Nalika.
Alisema,kama itashindikana kumpata mtu mwenye sifa, basi ni vyema kumpa nafasi hiyo mwekezaji wa awali Kampuni ya Best Luxury Safaris ambaye ameonesha uwezo mkubwa wa kuendeleza utalii na kuchangia uchumi wa Tunduru.
Mkazi wa kijiji cha Milonde Said Mbalamahengo alisema,kwa muda mrefu hawajawahi kuona wageni wakifika kwenye vitalu vya uwindaji vilivyo chini ya Jumuiya hiyo,lakini baada ya Kampuni ya Best Luxury Safaris kuanza shughuli zake wameshuhudia wageni wengi wa ndani na nje ya Tanzania wanaofika kutembelea vitalu hivyo vya utalii wa uwindaji.
Ameiomba Bodi hiyo, kutowapa nafasi wawekezaji wenye Historia mbaya na wababaishaji bali wahakikishe wanampata mwekezaji kama alivyo Kampuni ya Best Luxury Safaris ambaye katika kipindi cha miaka mitano ametoa mchango mkubwa katika sekta ya utalii na kuchangia maendeleo kwa vijiji vinavyounda Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori Nalika.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nalika Said Masoud alisema,jumla ya makampuni manne yamejitokeza kuomba kuwekeza utalii wa uwindaji baada ya mwekezaji wa mwanzo muda wake kumalizika.
Alisema, katika mchakato huo wataangalia kumpata mwekezaji ambaye atalipa vizuri mapato ya Serikali, ya jumuiya na kusaidia shughuli za maendeleo kwenye vijiji vinavyounda jumuiya hiyo.
Ameipongeza Kampuni ya Best Luxury Safaris kwa kuchangia maendeleo katika vijiji mbalimbali na kuyataka makampuni mengine ya uwekezaji katika sekta ya utalii kuiga utendaji nzuri na ushirikiano mkubwa kwa jamii.
Alisema, katika kipindi kifupi imetoa mchango mkubwa katika shughuli na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo katika sekta ya afya na elimu katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kalulu Mbale Motamota alisema,kwa sasa wapo mahali pazuri ikilinganisha na walipotoka,lakini ameonesha wasiwasi wake juu ya mchakato wa kumpata mwekezaji mpya ambaye anaweza kurudisha nyuma juhudi kubwa zilizoanza kufanywa na Serikali ya awamu ya sita kuimarisha sekta ya utalii.
Motamota alisema,katika mchakato huo unaotarajiwa kuhitimisha wiki ijayo kuna waombaji ambao hawafai kutolea mfano Kampuni ya Safari Shallom inayomilikiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Ryan Shallom ambaye amewahi kuwa mwekezaji katika vitalu mbalimbali hapa nchini,lakini Histori ya uwekezaji wake ni mbaya.
Alisema, mwaka 2021 amewahi kuwa mmoja wa wasimamizi wa kambi za uwindaji wa kitalii za Kampuni ya Best Luxury Safaris ambayo ilikuwa mwekezaji wao na yeye kama msimamizi alifanya mambo mengi mabaya ikiwamo kutolipa fedha za wafanyakazi,kuuwa wanyama bila vibali na kugawa nyama hizo kwa wananchi kama rushwa ili wamsaidie kukubalika kuwa mwekezaji mpya.
Aidha alisema,Shallom amehusika kutoa rushwa za fedha kwa baadhi ya viongozi wa Jumuiya na vijiji, hali iliyopelekea kukamatwa na maafisa waTaasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(Takukuru)wilayani Tunduru.
“nimewahi kupokea malalamiko ya wananchi wapatao 25 kutoka kwenye vijiji vinavyounda Jumuiya ya Nalika wakilalamikia kutolipwa mishahara yao na walikuwa wanajiandaa kwenda kudai haki zao kwa nguvu,jambo ambalo lilikuwa linakwenda kuleta uvunjifu wa Amani”alisema.
Aliongeza kuwa,kama Diwani alijaribu kutatua tatizo hilo bila mafanikio kutokana na usumbufu wake hadi alipoomba msaada kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru ambaye alisaidia kumaliza tatizo hilo.
Motamota,ameiomba Serikali,bodi ya ushauri ya mambo ya maliasili wilaya,Jumuiya ya Nalika pamoja na kamati ya mchakato wa kupatikana kwa mwekezaji mpya waepuke kuwaleta wawekeza wenye sifa hizo ambao watasababisha matatizo na migogoro mikubwa kwa jamii na serikali.
“naomba sana bodi ya ushauri,jumuiya ya Nalika wafanye uchambuzi wa kina ili watupatie mwekezaji bora atakayefanya utalii wetu uendelee badala ya kutuingiza kwenye migogoro na kuua utalii wetu unaokuwa kwa changamoto nyingi”alisema Motamota.
Alipotafutwa Shallom ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo hakuweza kupatikana kwa kuwa anaishi mkoani Mororogoro, na hata alipotafutwa kwa simu ya mkononi hakuweza kupatikana kwa kuwa simu zake zinashikiliwa na Takukuru kwa ajili ya uchunguzi.
Hata hivyo gazeti hili lilimtafuta Wakili wa Shallom, Wakili Ismail Kaukuya ambaye naye alidai mteja wake hapatikani kwenye simu yake ya mkononi na kwamba anaendelea kumtafuta kwa mawasiliano zaidi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.