Wakulima wa mbaazi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wamepata dhamana ya kuuza mbaazi kilo1,223,665, zenye thamani Zaidi ya bilioni 2.5 katika mnada wa pili wa mbaazi msimu wa 2023/2024.
Operesheni meneja Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU LTD), Ndg. Marcelino Mrope amesema kwamba, tani 839 zenye thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zilikusanywa katika mnada wa kwanza wa mbaazi kwa msimu huu. Ameyasema hayo wakati wa mkutano wa uuzaji wa mbaazi katika mnada wa pili Kijiji cha Msinji.
“Tulifanikiwa kukusanya tani 839 katika mnada wa kwanza wa mbaazi kwa msimu huu na kuuza mbaazi zetu kwa bei ya wastani shilingi 2,016 na kufanya zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kuingia katika mzunguko wilaya ya tunduru”. Alisema
Katika mnada wa pili msimu huu wa mbaazi wanunuzi 15 wamejitokeza kuweka zabuni kununua mbaazi kilo 1,223,665, ambapo wanunuzi watano walifanikiwa kununua mbaazi zote zilizopo ghalani kwa bei ya juu shilingi 2,085 na bei ya chini shilingi 2,075 na kufanya bei wastani kuwa 2,079, ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.5 zimeingia katika mzunguko wilaya ya Tunduru. Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika Tunduru (TAMCU LTD) Ndg. Mussa Manjaule wakati akitangaza bei ya mbaazi katika mnada wa pili wa mbaazi.
Aidha Ndg manjaule amewasihi wakulima wilaya ya Tunduru kuwa fedha hizi wanazozipata waendelee kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kuwa kilimo ni muhimili muhimu wa uchumi katika wilaya yetu ya Tunduru na kuwaomba kuendelea kulima Zaidi mazao hayo mbadala ya uchumi.
“Fedha tunazozipata tukawekeze, sisi kama wakulima ili tufikie lengo la kupandisha uchumi wa wilaya yetu”
Mnada wa tatu wa zao la mbaazi katika wilaya ya Tunduru unatarajiwa kufanyika mnamo Agosti 31,2023 katika Kijiji cha Angali
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.