WILAYA ya Tunduru mkoani,imepokea jumla ya Sh.bilioni 1,224,600,000.00 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuboresha upatikanaji wa fursa sawa katika ujifunzaji bora kwa elimu ya awali na msingi Tanzania Bara(Boost).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro,wakati akizindua ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa katika shule ya msingi Tinginya kata ya Tinginya vinavyojengwa chini ya mradi huo maalum.
Alisema,fedha hizo zitatumika kujenga ofisi za walimu,matundu ya vyoo,vichomea taka na madawati na kumaliza kabisa changamoto ya miundombinu kwenye shule za msingi wilayani Tunduru ambazo nyingi zimejengwa miaka ya zamani.
Alisema,shule hizo zitakuwa za mfano kutokana na ubora wake na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya awali na msingi wilayani humo.
Kwa mujibu wa Dc Mtatiro ni kwamba Serikali ya awamu ya sita imeanza kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule zote za umma ili ziwe bora na rafiki kwa wanafunzi na walimu.
Mtatiro,amehaidi kusimamia matumizi ya fedha zote na atahakikisha miundombinu inajengwa kwa ubora wa hali ya juu ili ilingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na kuwaonya wasimamizi na watekelezaji wa miradi kutothubutu kuchezea fedha wala vifaa vitakavyoletwa kwa ajili ya kazi.
Pia alisema,ameagiza miradi yote itakayotekelezwa katika wilaya hiyo kwa njia ya force akaunti ifanywe na mafundi kutoka eneo husika na kazi za kufyatua tofali zifanywe na vijana wa jeshi la akiba(mgambo), badala ya kuwatafuta watu kutoka nje ya Tunduru.
Alisema,hatua hiyo itasaidia sana miradi inayojengwa kulindwa kwa kuwa wananchi wataiona ni yao na hivyo kusimamiwa kwa karibu na jamii itafaidika na uwepo wa miradi hiyo kwa kufanya kazi za kuwaingizia kipato.
Katika hatua nyingine,Mtatiro amewaasa wananchi hasa vijana kutokubali kurubuniwa na baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema na serikali kwa kuwashawishi kukataa kushiriki na kufanya kazi za kujitolea katika maeneo yao.
Amewataka wananchi wa Tinginya na vijiji vingine wilayani humo, kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na serikali iliyopo madarakani katika ujenzi wa miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake mratibu elimu kata ya Tinginya Rashid Chalamanda alisema,wamepokea kiasi cha Sh.milioni 331,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa tisa kati ya hayo mawili kwa ajili ya elimu ya awali,matundu ya choo,jengo la utawala na kichomea taka.
Alisema,ujenzi wa madarasa hayo utasaidia sana kumaliza changamoto ya mlundikano wa watoto madarasani na kushawishi kupenda shule na hivyo wilaya hiyo kupiga hatua kielimu kama ilivyo katika maeneo mengine hapa nchini.
Diwani wa kata ya Tinginya Eliasa Pelemende alisema,wananchi wa kata hiyo wako tayari kushiriki na kujitolea nguvu zao katika ujenzi huo ili kazi ikamilike haraka.
Mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Tinginya Maliche Mohamed,ameishukuru Serikali kuwajengea vyumba vipya vya madarasa ambavyo vitamaliza kero ya kukaa wanafunzi wengi katika chumba kimoja.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.