WAKALA wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imepokea zaidi ya Sh.bilioni 1 zilizotolewa na serikali kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 kutekeleza miradi miwili ya maji katika kijiji cha Daraja mbili na Kazamoyo.
Akizungumza ofisini kwake,Meneja wa Ruwasa wilayani Tunduru Silvia Ndimbo alisema,mradi wa kijiji cha Darajambili umetengewa jumla ya Sh. milioni 598,556,400 na utakapokamilika utaweza kuhudumia kaya 243 zenye wakazi 2,000.
Aidha alisema, katika mradi wa Kazamoyo fedha zilizotengwa ni Sh.476,578,000 na miradi hiyo itakapokamilika itamaliza kabisa changamoto ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji hivyo viwili.
Alisema, apo awali vijiji hivyo havikuwa na huduma ya maji safi salama, badala yake wananchi walitegemea na kutumia visima vya asili ambavyo maji yake sio safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Amewaomba wananchi ambako Serikali kupitia Ruwasa inaendelea kutekeleza miradi ya maji, kuhakikisha wanalinda miundombinu,kutunza vyanzo vya maji na kuchangia huduma za maji kwa miradi inayoendelea iliyoanza kufanya kazi na ile inayotarajia kujengwa ili iweze kuwa endelevu.
Alisema,ni muhimu wananchi kuchangia huduma ya maji kwa sababu ni kama huduma nyingine katika kijamii zinazopaswa kuchangia ili miradi hiyo iweze kudumu na kuleta tija katika jamii.
Katika hatua nyingine Ndimbo alisema, wilaya ya Tunduru ina vijiji zaidi ya 157 kati ya hivyo, vijiji 142 vinahudumiwa na Ruwasa ambapo vijiji 113 sawa na asilimia 79 vinapata huduma ya maji safi na salama na vijiji 29 vilivyobaki vinahudumiwa na Mamlaka ndogo ya maji Tunduru(Tuwasa).
Alisema, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Ruwasa iliweza kutekeleza miradi 8 ya maji katika vijiji 12 kwa gharama ya Sh.bilioni 1.2 na mwaka 2021/2022 wameanza kutekeleza miradi mingine 6 ambayo iko hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mkandarasi anayejenga mradi wa maji Darajambili Stanley Mlelwa alisema,walianza utekelezaji wa mradi huo mwezi Januari na wanatarajia kukamilisha April na hadi sasa umefikia asilimia 15 ya utekelezaji.Alisema, wako nyuma ya mudakutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa tofali ambazo zinapatikana mbali,lakini amehaidi kufanya kazi usiku na mchana ili kumaliza kazi hiyo na ameiomba Serikali kuwaamini kwa kuwapa kazi wakandarasi wa Kitanzania katika kujenga miradi mbalimbali.Akiongea kwa niaba ya wananchi wenzake Ali Sued ameishukuru sana Serikali kwa kupeleka mradi wa maji ambao unakwenda kumaliza kabisa changamoto yam aji katika eneo hilo.
Pia alisema, mradi huo umewasaidia kupata kazi zinazowaingizia fedha za kujikimu na familia, na kuiomba Serikali kupeleka miradi mingine katika kijiji hicho ambacho bado kiko nyuma kimaendeleo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.