WAKALA wa Barabara Tanzania(TANROADS) Mkoa wa Ruvuma, iko katika hatua ya mwisho kuanza ujenzi wa Barabara ya mchepuko( Songea ByPass)maarufu kama (Mtwara Corridor)yenye urefu wa km 14.3.
Meneja wa TANROADS mkoani Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi alisema,barabara hiyo ni sehemu ya ujenzi wa mradi wa Barabara kuu ya Songea-Makambako.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mlavi ni kwamba,ujenzi wa Barabara hiyo itaanzia eneo la Namanditi ambapo itapita kata ya Mwenge msindo,Msamala, kituo cha kupoza umeme Unangwa hadi Changarawe Barabara kuu ya Songea-Tunduru.
Aidha alisema,katika mradi huo kutakuwa na eneo la mzunguko (round about) tatu ya kwanza itejengwa eneo la Namanditi,ya pili Msamala karibu na kituo cha mafuta cha Ottawa na nyingine itajengwa eneo la Changarawe Barabara kuu ya Songea-Tunduru.
Alisema, pindi Barabara hiyo itakapojengwa itasaidia sana kuondoa changamoto ya msongamano wa magari katikati ya mji wa Songea hasa malori yanayobeba makaa ya mawe na itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi.
“Barabara hii ya mchepuko(Songea Bypass) ina umuhimu mkubwa na itaongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma na wale wanaofika kutoka mikoa mingine ya jirani”alisema Mlavi.
Kwa mujibu wa Mlavi, tathimini ya fidia kwa ajili ya kuwalipa wananchi watakaopitiwa na mradi huo imeshafanyika na sasa Serikali iko katika hatua ya mwisho ya malipo ili wananchi waweze kupisha ujenzi wa mradi huo.
Mhandisi Mlavi, amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla kuiamini Serikali yao kwani imejipanga vyema kwa ajili ya kutekeleza mradi huo na miradi mingine katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
“nachukua nafasi hii kuwatoa wasiwasi wananchi kuhusu ujenzi wa Barabara hii kwani serikali iko kazini na imejipanga kuhakikisha itajengwa kwa kama ilivyokusudia”alisema Mlavi.
Naye Mhandisi Izaki Issa kutoka ofisi ya meneja wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS)mkoa wa Ruvuma alisema, Barabara hiyo ya mchepuko itapita katika vijiji vitano vya Namanditi,Luwawasi,Mtaungana,Osterbay na Kuchile.
Baadhi ya wananchi,wameiomba Serikali kuanza ujenzi wa Barabara hiyo haraka ili iweze kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Ruvuma na kuharakisha maendeleo yao.
Mariam Mwela mkazi wa Namanditi alisema, wameupokea mradi huo kwa mikono miwili kutokana na faida zake kiuchumi na ameipongeza TANROADS mkoa wa Ruvuma kufikiria kujenga Barabara ya mchepuko katika mji wa Songea.
Aidha,ameiomba Serikali kuwalipa fidia zao mapema ili wakatafute maeneo mengine ya kuishi,kwani tangu TANROADS ilipoweka alama za X kwenye nyumba zao wanashindwa kuendeleza maeneo yao na wanaishi kwa hofu kubwa.
Pascal Msigwa(Top One)alisema,mradi huo ni muhimu sana kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na kuipongea serikali ya awamu ya sita kwa kuonyesha nia ya kujenga Barabara hiyo na Barabara kuu ya Songea-Makambako.
Rajabu Kanganya mwendesha boda boda, ameiomba Serikali kupitia TANROADS mkoa wa Ruvuma,kuhakikisha mradi huo unaanza haraka badala ya kuchukua muda mrefu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.