WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II katika ziwa Nyasa ambayo itakuwa inahudumia bandari zinazopita katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya,Ludewa mkoani Njombe na Nyasa mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya huduma za bandari katika ziwa Nyasa,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko anasema TPA inahudumia jumla ya bandari 15 katika ziwa Nyasa ambapo katika Mkoa wa Ruvuma,TPA inahudumia bandari sita.
Anazitaja bandari za ziwa Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma kuwa ni Mbambabay,Liuli,Njambe,Lundu,Mkili na Ndumbi,katika Mkoa wa Njombe TPA pia inahudumia bandari sita ambazo ni Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde,Lupingu na Manda ambapo katika Mkoa wa Mbeya TPA inahudumia bandari tatu ambazo ni Itungi,Kiwira na Matema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA,baadhi ya bandari TPA imeweka miundombinu ya kisasa,pia kuna bandari ambazo zinaendelea kuwekwa miundombinu kwa ajili ya utoaji huduma bora na za kisasa katika bandari hizo.
“Kila bandari inahitaji kuwa na magati,maghala,yadi za kutunzia mitambo na mizigo na uwepo wa nyumba za kuishi wafanyakazi,sanjari na kuweka mifumo ya zimamoto,majisafi,maji taka na mifumo ya TEHAMA ili kufanyakazi kwa ufanisi na tija kulingana na maelekezo ya serikali’’,anasisitiza Mhandisi Kakoko.
Anasisitiza kuwa katika miaka mitano ijayo TPA imejipanga kukamilisha miundombonu na mifumo yote kwenye bandari zote 15 zilizopo katika ziwa Nyasa.
Akizungumzia utendaji kazi wa TPA katika ziwa Nyasa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Mhandisi Kakoko anazitaja shehena kuu zilizokuwa zinasafirishwa kuwa ni makaa ya mawe ambayo yalikuwa yanapakiwa kutoka bandari za Ndumbi na Mbambabay na kusafirishwa hadi bandari ya Kiwira Kyela mkoani Mbeya.
Anasema katika kipindi hicho,TPA pia iliweza kusafirisha saruji,mabati,dagaa,sukari na mizigo mingine ambapo kwa kipindi cha miaka sita iliyopita ilisafirishwa shehena ya mizigo zaidi ya tani 4500 kwa mwaka.
Hata hivyo anasema kwa ujumla kulikuwa na ongezeko la tani 9000 kutoka tani 2233 ya mwaka 2014/2015 hadi tani zaidi ya 11,000 mwaka 2019/2020.
Mhandisi Kakoko anasisitiza kuwa ili kuboresha huduma katika bandari zote za ziwa Nyasa,TPA inatekeleza mpango kabambe unaoanza mwaka 2021/2022 na unaotarajia kukamilika katika kipindi cha mwaka 2028/2029.
“Mpango huo kabambe utaongeza shehena ya mizigo katika ziwa Nyasa kutoka tani zaidi ya 11,000 hadi kufikia shehena ya mizigo zaidi ya tani 100,000,lengo hili linachochewa na mipango mizuri ya serikali ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami toka Mbinga hadi Mbambabay’’,anasisitiza Mhandisi Kakoko.
Anasema kutokana na kukamilika kwa lami ya Mbinga hadi Mbambabay na kuanza kutoa huduma za meli katika ziwa Nyasa kutafufua uchumi wa mji wa Mbambabay hivyo kuunganisha Tanzania kupitia ushoroba wa Mtwara na nchi za Malawi,Msumbiji na Zimbabwe na Zambia.
“Mji wa Mbambabay utafufuka kwa kasi,TPA inafanya usanifu wa bandari zote zilizopo katika ziwa Nyasa na kwa kweli tunashirikiana na nchi jirani ya Malawi ili wakati tunaendeleza bandari za Tanzania,tuendeleze pia bandari za Malawi,pia tunafanya kampeni za masoko katika nchi za Malawi na Msumbiji’’,anasema.
Akizungumzia kuhusu meli mpya katika ziwa Nyasa,Mkurugenzi huyo anasema ziwa Nyasa sasa lina meli tatu zinazomilikiwa na serikali kati ya hizo meli mbili za MV Njombe na MV Ruvuma ni za mizigo na meli moja ya MV Mbeya II ni ya abiria.
Anasema katika kipindi cha miaka sita iliyopita kwa wastani kwa mwaka kulikuwa na abiria 4917 amesema kumekuwa na ongezeko la abiria katika mwaka 2019/2020 toka abiria 894 mwaka 2018/2019 hadi abiria 3867 mwaka 2019/2020 baada ya kujitokeza meli ya abiria ya MV Chambo ya Msumbiji ambayo iliacha kutoa huduma baada ya kuzuka kwa COVID 19.
Hata hivyo anasema idadi ya abiria inatarajia kuongezeka katika ziwa Nyasa baada ya kuzinduliwa kwa huduma ya meli ya abiria ya MV Mbeya II ambayo itawezesha kusafirisha abiria zaidi ya 12,000 kila mwezi.
Akizungumzia gharama za meli zote tatu katika ziwa Nyasa,Mkurugenzi Mkuu wa TPA anasema zaidi ya shilingi bilioni 20.1 zimetolewa na serikali kujenga meli zote tatu na kwamba meli hizo zimetengenezwa na kampuni ya Songoro Marine inayomilikiwa na Mtanzania.
“Meli mbili za mizigo MV Njombe na MV Ruvuma kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1000 na kwamba kila meli imegharimu shilingi bilioni 5.5 na meli ya abiria ya MV Mbeya II ina uwezo wa kubeba abiria 300 na mizigo tani 200, imegharimu shilingi bilioni 9.1’’,anasema.
Kwa mujibu wa Kakoko meli ya abiria ya MV Mbeya II imerithi jina la meli ya MV Mbeya I iliyozama eneo la Makonde ziwa Nyasa mwaka 1977.
Hata hivyo anasema meli ya MV Mbeya II baada ya kujengwa iliingizwa majini Septemba 2019 na kwamba kwa kuwa meli ni chombo ambacho kinatakiwa kuwa na usalama wa kutosha kilikaguliwa kimataifa na kupata kibali cha Mamlaka inayosimamia usalama wa vyombo vya majini na kuanza safari Oktoba 20,2020.
Akizungumza baada ya kuzindua meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema wilaya ya Nyasa sasa imefunguka kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami toka Mbinga hadi Mbambabay na kuanza rasmi kwa huduma za meli tatu ndani ya ziwa Nyasa.
Mwandishi ni Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.