UWANJA wa ndege wa Songea umefunguliwa baada ya kukamilika ujenzi wake kwa asilimia 50 na ndege kubwa aina ya Bombadier zinatarajia kuanza kutua Agosti mwaka huu.
Akitoa taarifa ya ukarabati wa uwanja huo kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Mshauri ujenzi wa uwanja wa Songea, Jofrey Keneth amesema wamefikia hatua nzuri ya ujenzi wa uwanja huo hivyo kuruhusu ndege kuanza kutua.
“Hivi sasa ndege ndogo zinatua kwenye uwanja mpya ambao umefunguliwa,uwanja umejengwa kwa mita 800 na Mkandarasi ataongeza mita nyingine 400 ambazo zitaleta jumla ya mita 1200 hivyo kuwezesha kuruka na kutua ndege kubwa aina ya bombadier’’,alisema.
Amesema Mkandarasi ameahidi kwamba hadi kufika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu atakuwa ametimiza kujenga uwanja kwa mita 1200 ambazo ndizo hitaji la chini zaidi kuwezesha kutua ndege aina ya bombardier.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa uwanja huo ambao unakarabatiwa na Kampuni ya CHICCO kutoka nchini China,Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Lasack Alinanuswe,amesema serikali imetoa kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni 39 kutekeleza mradi huo ambao mkataba wake ni miezi 20 inayoishia Desemba 28 mwaka huu.
Amesema mradi huo tangu kuanza kutekelezwa umeweza kutoa ajira kwa wafanyakazi 110 ambao wote ni watanzania kutoka mkoani Ruvuma na wachina saba.
“Mhandisi wa ujenzi huo hivi sasa anafanyakazi usiku na mchana ili aweze kukamilisha kazi hiyo ndani ya mkataba,Juni 28 mwaka huu tulihamisha shughuli za urukaji wa ndege kutoka upande wa zamani wa 14 kwenda upande mpya wa 32 kwa hiyo hivi sasa ndege zinatumia uwanja mpya’’,alisema.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo kwa niaba ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma,Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa Musa Homera amesema wakazi wa Ruvuma wanalalamika kupanda ndege kwa gharama kubwa toka Songea hadi Dar es salaam ambapo wanalipa nauli ya shilingi milioni moja kwenda na kurudi.
Amesema nauli ya ndege za serikali ni gharama nafuu hivyo ni matarajio ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma,kuona sasa Songea inafunguka kupitia usafiri wa anga ambao watu wengi wanaweza kumudu.
“Hivi sasa Songea imejifunga,hatuwezi kupokea wageni toka mbali,watu wanashindwa kusafiri kwa njia ya barabara ambayo ni zaidi ya saa 15 toka Dar es salaam hadi Songea,lakini usafiri wa ndege ukianza watu watanufaika wakiwemo wagonjwa’’,alisisitiza Homera.
Amesema Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Ruvuma,inahimiza uwanja wa ndege wa Songea ufunguliwe sio kwa sababu kupenda anasa bali ni mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na nchi jirani za Msumbiji na Malawi.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Nuru Ngereja amesema Kamati ya Siasa ya CCM ingetamani miradi yote ikamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu kwa kuwa serikali iliahidi na imetekeleza.
Uwanja wa ndege wa Songea ulijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 umewekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira yote masika na kiangazi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 9,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.