KITUO cha Uhamiaji cha Mkenda kilichopo wilayani Songea mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kimeweza kuhudumia raia wa kigeni na watanzania wapatao 174 katika kipindi cha kuanzia Aprili Mosi hadi 27,2020.
Akitoa taarifa ya kituo hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipofanya ziara ya kutembelea kituo hicho,Afisa Uhamiaji Kituo cha Mkenda Inspekta Ambinga Swai amesema kati ya wageni waliohudumiwa katika kipindi hicho ni raia wa Tanzania walioingia nchini ni 73,raia wa Tanzania waliotoka nchini ni 44,raia wa kigeni walioingia nchini 17 na raia wa kigeni waliotoka nchini ni 40.
Hata hivyo Swai amesema raia wa kigeni na watanzania waliotoka nje ya nchi na kuingia nchini walianza kupelekwa katika eneo la karantini lililopo Peramiho nje kidogo ya Mji wa Songea kuanzia Aprili 6 na kwamba hadi kufikia Aprili 27 jumla ya watu 92 walikuwa kwenye karantini.
Amesema kati ya watu hao raia wa Tanzania ni 82 na raia wa kigeni 10 na kwamba katika idadi ya waliopelekwa karantini kulikuwa na Mkisiwa mmoja ambaye ni raia wa Tanzania.
Akizungumza baada ya kukagua kituo hicho Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa ,kazi nzuri na kutahadharisha katika kipindi hiki cha vita ya corona kuchukua tahadhari ambapo amekemea wasishiriki katika vitendo vya rushwa kujaribu kuwapitisha wageni wanaotoka nje ya nchi bila karantini.
Amewashauri kuchukua tahadhari zilizotolewa na watalaam wa afya ikiwemo kunawa mikono,matumizi ya vitakasa mikono na matumizi ya barakoa na kwamba raia wote wanaoingia nchini lazima wawekwe karantini kwa siku 14.
“Wapimeni wageni wote wanaongia nchini awe ni Mtanzania au raia wa kigeni ,tumewaleta thermal scanner,ugonjwa huu ni hatari,nichukue fursa hii kuwapongeza watumishi wote wa afya ambao wamesimama imara,nakuomba Mganga Mkuu angalia maslahi ya watumishi wa afya’’,alisisitiza.
Amesema kila mmoja akiwajibika na kushirikiana kwa pamoja vita ya corona tutaishinda na kwamba kumuumba Mungu katika janga hili kuende sanjari na juhudi za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ametoa shilingi 500,000 kama motisha kwa askari watano wanaolinda eneo la mpaka wa Mkenda ili kuhakikisha kuwa nchi na Mkoa wa Ruvuma unaendelea kubaki katika hali ya usalama.
Kituo cha uhamiaji Mkenda chenye Taasisi tano kipo umbali wa kilometa 140 kutoka mjini Songea,kituo hicho ambacho kimepakana na nchi ya Msumbiji kilianza kufanyakazi tangu mwaka 2009.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma.
Aprili 29,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.