KAMISHINA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu ambae ni k Mary Longway amefungua mkutano wa wadau wa uchaguzi Mkoa wa Ruvuma uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Akizungumza mbele ya waandishi wa Habari,Wakati wa kufungua mkutano huo Longway amesema Tume ya Taifa kutokana na sheria ya uchaguzi sura ya 343 imepewa mamlaka ya kutoa Elimu ya mpiga kura nchi nzima,kuratibu na kusimamia asasi Zinazotoa Elimu hiyo.
Vilevile, amesisitiza umuhimu ushirikishwaji wa wadau wa uchaguzi kupitia mawakala wa vyama vya siasa, kwa sababu siku ya uchaguzi vyama vya siasa vimepewa nafasi ya kuweka wakala katika Kila kituo cha kupigia kura.
"Tume inawahakikishia wananchi kuwa imejipanga katika kusimamia uchaguzi wa mwaka huu kwa kufuata katiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali na Tume inaamini kuwa Kila mdau akitimiza wajibu wake kwa kufuata taratibu, watanzania wataweza kupiga kura kwa amani siku ya uchaguzi", amesema Longway.
Kwa upande wake Afisa Uchaguzi Mkoa wa Ruvuma Happy Msanga amesema Tume inawatoa hofu wapiga kura wote wenye mahitaji maalumu kwa kuwa maelekezo yametolewa kwa watendaji wa uchaguzi kutoa kipaumbele kwa watu wanaoishi na ulemavu, wajawazito, akina Mama wanaonyonyesha waliokwenda na watoto vituoni, wazee na wagonjwa.
Amesisitiza kuwa Tume imewaangalia watu wote uhitaji maalumu wataweza kupiga kura kutokana na uhitaji wake na kwamba matarajio ya Tume ni kuona Kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura anajitokeza na kadi yake ya kupiga kura katika kituo alichojiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi ya kikatiba.
Askofu wa Kanisa la kirutheri Dayosisi ya Mkoa wa Ruvuma Amon Mwenda amesema yeye Kama kiongozi wa dini ni wajibu wake kutoa Elimu ya uchaguzi kwa wananchi kwa sababu ni sehemu ya utume wake kutokana nafasi aliyonayo anakutana na watu mbalimbali kwa muda tofauti.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Wasaidizi was Sheria ( Songea Paralegal Centre) Fatma Missango amesema wamepewa thamani kubwa sana na Tume ya uchaguzi kwenda kutoa mafunzo kwa Umma kwa watu wengi ambao hawana uelewa kuhusu uchaguzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Huru la Wazee Manispaa ya Songea Elzear Nyoni amesema Elimu ambayo wamepata wao Kama wadau wa uchaguzi ni muhimu kwenda kuifikisha Kwa wadau wa uchaguzi hawa makundi yenye mahitaji maalum kama wazee na watu wenye ulemavu.
Imeandaliwa na Farida Mussa
Ofisi ya Habari ya Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 3,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.