Jiwe la Litembo lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma,lina utajiri wa utalii wa kishujaa na kihistoria kutokana na mababu na mabibi zetu takribani 800 waliuwawa na wakoloni wa kijerumani Machi 4,1902.
Mashujaa hao waliuawa kikatili katika vita ambayo walikataa kutawaliwa na mkoloni wa kijerumani.Jiwe ambalo yalifanyika mauaji hayo ambayo yalikuwa makazi yao linaitwa Litembo kutokana na kufanana sana na kichwa cha mnyama tembo.
Eneo hilo lenye kichwa kinachofanana na tembo ndiyo yalikuwa makazi na maficho ya wazee wakati wa vita dhidi ya wajerumani ambapo ndani ya jiwe hilo kuna pango refu linalotokea katika Kijiji cha Maguu wilayani Mbinga.Inaelezwa ndani ya pango hilo kuna Wanyama wakali,nyoka,maji mengi,pia inadaiwa kuna madini ya zebaki na samani za chuma.
Katibu wa Baraza la Mila na Utamaduni Kata ya Litembo Bruno Tembo anasema mashujaa hao 800 baada ya kuuawa walizikwa katika makaburi ya Pamoja ya watu 25 katika Kijiji cha Litembo na kwamba ili kuwakumbuka mashujaa hao mnara wa makumbusho umejengwa kwenye maeneo ya jiwe la Litembo na kwamba kila mwaka Novemba 28 katika mnara huo yanafanyika maadhimisho ya kuwakumbuka wazee 800 waliopambana na wajerumani.
Kijiji cha Litembo pia kimepewa jina la jiwe hili ambalo lina pango refu ambalo mababu zetu walionusurika kwenye vita hiyo waliingia kwenye pango na kutokea upande wa pili wa jiwe hilo.
Katibu huyo wa Baraza la Mila na Utamaduni anabainisha kuwa kiongozi wa wajerumani aliyeitwa Korongo kutokana na ukatili wake alimtumia ujumbe kiongozi wa kabila la wamatengo mwaka 1902 kuwa anataka kuingia katika eneo hilo na kuwataka viongozi hao wa jadi kumuunga mkono ili kuwa chini yake.
Anasimulia zaidi kuwa kiongozi wa wamatengo baada ya kupata ujumbe huo alipiga ngoma kubwa kwa ajili ya kuwakusanya wananchi ambao aliwaeleza kuhusu ujumbe huo wa Korongo ambapo kwa pamoja wananchi hao walikataa kuwa chini ya wakoloni wa kijerumani.
Kutokana na maamuzi hayo ya wazee Korongo wa Kijerumani aliamua kuwapeleka wapiganaji wake wakiwa na bunduki 19 ili kupigana na mashujaa wa kabila la wamatengo.
Mababu zetu hawakuogopa walijipanga wakiwa wamejitokeza kwa mamia kwa kutumia silaha za jadi walijipanga nyuma ya jiwe la Litembo na kuanza kupambana na wakoloni wa kijerumani,hata hivyo wajerumani walitumia risasi za moto kuwauwa mashujaa 800 kikatili.
“Damu za mashujaa wa kabila la wamatengo waliouwawa na wajerumani zilichuruzika kwenye mto Mapipa ambao unaanzia kwenye milima ya Umatengo hadi kwenye ziwa Nyasa.Mashujaa walionusurika waliingia kwenye pango la jiwe la Litembo ambalo linachukua saa nne na kutokea upande wa pili katika Kijiji cha Maguu’’,anasema Tembo.
Hata hivyo Tembo anasema kiongozi wa wajerumani baada ya kuwauwa mashujaa 800 akiwa na wenzake aliamua kuchoma nyumba zote moto pamoja na vyakula vyote viliteketezwa na kufanya uharibifu mkubwa katika eneo hilo la wamatengo.
Salvius Nyamajabeni ni Mwenyekiti Baraza la Mila na Utamaduni wa kabila la wamatengo aliyechaguliwa tangu mwaka 1958 anasema, mara baada ya mashujaa hao kuuwawa walizikwa katika makaburi ya Pamoja ambapo kila kaburi walizikwa mashujaa zaidi ya 25 kishujaa katika eneo la Litembo.
Afisa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema,wamedhamiria kuvitangaza vivutio vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo eneo la Litembo ili watalii wengi waweze kufika na kuona namna mababu zetu walivyoshiriki katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni wa kijerumani.
Makala imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Novemba 23,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.