Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameshiriki maadhimisho ya utoaji tuzo kwa walipakodi bora Mkoani Ruvuma,
Kanali Abbas ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuhamasisha ulipaji wa kodi stahiki, na kuwashukuru wafanyabiashara kwa kujitolea katika kutoa michango ya kodi.
Katika hafla hiyo, Kanali Abbas amesema wafanyabiashara hao wameonesha uzalendo kwa Taifa na kuwaomba waendelee kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ili waweze kujifunza kutoka kwao.
Amesisitiza umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi.
"Mahusiano mazuri kati ya TRA na wafanyabiashara yanajenga msingi wa ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati, jambo litakalowezesha Serikali kutimiza majukumu yake," alisema Kanali Abbas.
Aidha, amewakumbusha wafanyabiashara kutoa na kudai risiti sahihi, kwani Serikali inapata mapato kupitia risiti hizo.
Amewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na kujiepusha na vitendo vya ukwepaji kodi, huku akisisitiza kwamba elimu ya kodi inapaswa kuendelea kutolewa, ikizingatiwa kuwa idadi ya walipakodi inaongezeka kila siku.
Kanali Abbas ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili walipakodi na kutoa elimu endelevu ili kila mfanyabiashara atimize wajibu wake bila usumbufu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.