WAKAZI 1,138 WANUFAIKA NA MRADI WA MAJI MUHUKURU SONGEA
WAKALA wa Maji na usafi wa mazingira RUWASA wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametekeleza mradi wa maji mtiririko wa Muhukulu kwa thamani ya sh.milioni 138 ambao utawanufaisha wakazi 1,138.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma, Meneja wa RUWASA wilaya ya Songea Mhandisi Samwel Sanya amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kuvihudumia vijiji vya Muhukuru, Lilai,Mkayukayu na Muhukuru barabarani.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2014 na wafadhili kutoka Abasia ya Hanga kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vya Lilai na Muhukuru barabarani ambapo ujenzi wa matanki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 50,000 na lita 75,000 ulifanyika.
Sanya amezitaja kazi nyingine zilizofanyika katika utekelezaji wa mradi huo kuwa ni kuchimba mtaro na kulaza bomba kuu la kusambaza maji umbali wa kilometa tatu,kujenga vituo 14 vya kuchotea maji katika kijiji cha Lilahi na vituo vitatu katika kijiji cha Barabarani.
“Sisi kama RUWASA tumechimba mtaro wa kusambaza maji katika vijiji vya Lilahi na Barabarani umbali wa kilometa 24.6,ujenzi wa vituo kumi vya kuchotea maji kijiji cha Lilahi,ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji na ujenzi wa chemba kwa ajili ya mita’’,alisema Mhandisi Sanya.
Hata hivyo Sanya amesema hadi sasa maji yanapatikana katika vituo 40 na kwamba RUWASA inaendelea na kazi ya kuunda jumuiya za watumia maji kwa kufuata sheria namba tano ya mwaka 2019 kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za maji zinasimamiwa vizuri na wananchi wenyewe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ameipongeza serikali kwa kutoa fedha ambazo zimetekeleza mradi huo ambapo ametoa rai kwa wananchi kulinda miundombinu ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Naye Felista Nyoni mkazi wa Muhukuru amesema kabla ya serikali kuwapatia maji ya bomba,walikuwa wanasafiri kila siku umbali wa saa tano kwenda na kurudi kutafuta maji ambapo hivi sasa changamoto ya maji imebaki kuwa historia.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 13,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.