Zaidi ya wakazi 6,000 wa vijiji vya Kilimasera, Ukiwayuyu, Mtakanini, Mterawamwahi, na Matependwe, wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, wanatarajia kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima virefu vitano.
Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeidhinisha Shilingi milioni 300 kwa ajili ya mradi huo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa uchimbaji wa visima 900 kwa kila jimbo nchini.
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Namtumbo, Salome Method, amesema uchimbaji wa visima hivyo ulianza Oktoba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Februari 2025.
“Kazi zilizopangwa ni uchimbaji wa visima, ujenzi wa vioski vya kuchotea maji, ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji, uwekaji wa matenki ya lita 10,000 kwa kila kijiji, ufungaji wa pampu za kusukuma maji na mifumo ya umeme wa jua,” alisema Method.
Aliongeza kuwa uchimbaji wa visima na ununuzi wa vifaa muhimu umekamilika, huku ujenzi wa vioski ukiwa umefikia zaidi ya asilimia 80.
Diwani wa Kata ya Ligera, Somebody Mhongo, ameishukuru serikali kwa kufanikisha mradi huo, hasa kwa kijiji cha Mterawamwahi ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikitegemea maji yasiyo safi kutoka mabonde na mito.
Mtendaji wa Kijiji cha Mterawamwahi, Joseph Haule, amesema kijiji hicho kinategemea mabomba mawili ya kupampu kwa mkono ambayo hayawezi kukidhi mahitaji ya wakazi wake.
Wakazi wa eneo hilo wameeleza kuwa tatizo la maji limeleta changamoto nyingi, ikiwemo migogoro ya ndoa kutokana na wake zao kuchelewa kurudi nyumbani wakisaka maji.
Lucy Mgala, mmoja wa wakazi, amesema wanawake hulazimika kwenda kuchota maji mtoni na mabondeni, jambo linalowakabili na hatari mbalimbali, hususan msimu wa masika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.