Wakulima wa zao la ufuta katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, wameandika historia mpya baada ya kuuza zaidi ya kilo milioni minne za ufuta kwa bei ya shilingi 2,450 kwa kila kilo kupitia mnada wa kwanza wa wazi wa kidigitali ulioendeshwa kwa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Soko la Pamoja la Bidhaa Tanzania (TMX).
Mnada huo umefanyika kwa uwazi mkubwa huku ukitumia teknolojia ya kisasa iliyolenga kuwanufaisha wakulima kwa kupata bei stahiki na kuondoa ulanguzi wa madalali waliokuwa wakiwanyonya kwa miaka mingi.
Katika hatua hiyo, wakulima walioshiriki mnada huo walionesha kuridhika na mafanikio ya mfumo huo wa TMX unaowaunganisha moja kwa moja na wanunuzi wakubwa bila kuhitaji wapambe wa soko.
Afisa Kilimo wa Wilaya ya Namtumbo, Ndg. Ambokile Paul, amesema mafanikio hayo ni ushahidi tosha kuwa teknolojia ikitumika ipasavyo, inaweza kuwa daraja la maendeleo kwa mkulima wa kawaida. Alibainisha kuwa kilimo cha ufuta sasa kinazidi kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa maelfu ya wakazi wa Namtumbo.
“TMX imeleta mapinduzi makubwa. Huu ni mfumo wa haki na uwazi, ambapo mkulima anaona kila hatua ya mnada na ana uhakika wa kupata malipo yake bila kuchelewa wala kupunjwa. Hii ndiyo njia ya kwenda mbele kwenye kilimo cha kibiashara,” alisema Afisa huyo wa kilimo kwa msisitizo.
Pamoja na mafanikio hayo, Afisa Kilimo huyo ametoa rai kwa wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao ili kuendana na mahitaji ya soko la kimataifa. Alisisitiza umuhimu wa kuvuna kwa wakati, kukausha vizuri na kufungasha kwa viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuongeza ushindani na kuvutia wanunuzi wa nje ya nchi, jambo ambalo linaweza kuongeza maradufu mapato ya wakulima.
Kwa mafanikio haya ya kihistoria, Wilaya ya Namtumbo sasa imejipambanua kama mfano bora wa mageuzi ya kilimo kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa. Kilimo cha ufuta kimeibuka kuwa si tu chanzo cha kipato, bali pia chombo cha kuinua hadhi ya mkulima na kuipa Tanzania heshima katika soko la dunia. Bila shaka, huu ni mwanzo wa enzi mpya ya kilimo cha kisasa chenye tija na faida kwa mkulima wa kawaida.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.