Na Albano Midelo,Songea
WAKULIMA mkoani Ruvuma hadi kufikia Juni 2023,wamefanikiwa kuvuna tani 1,870,800 za mazao ya chakula,biashara na bustani zilizolimwa katika hekta 897,171.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anazungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kilimo biashara yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Familia Takatifu Bombambili mjini Songea.
Amebainisha kuwa kati ya tani hizo,wakulima wamefanikiwa kuzalisha mazao ya chakula hekta 550,310 ambazo zimetoa mavuno tani 1,598,163 na kwamba katika mazao ya biashara wakulima wamezalisha hekta 332,459 ambazo zimetoa jumla ya tani 94,741.
“Katika msimu wa mwaka 2022/2023 Mkoa wetu ulilenga kulima hekta 930,082 za mazao ya chakula,biashara na bustani zilizotarajiwa kutoa mavuno ya tani 1,965,072,wakulima wamefikia lengo la kuzalisha kwa asilimia 97 na lengo la kuvuna kwa asilimia 95’’,alisema RC Thomas.
Hata hivyo amesema uzalishaji wa mazao uliofanywa na wakulima msimu huu unawahakikishia usalama wa chakula siyo tu katika Mkoa wa Ruvuma bali pia katika nchi nzima na kwamba Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa wa kwanza nchini kwa uzalishaji mazao ya nafaka.
Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ambapo katika msimu wa mwaka 2022/2023 Mkoa ulipokea mbolea ya ruzuku tani 83,207 ambazo zimechochea wakulima kuongeza uzalishaji.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewahamasisha wakulima kuanzisha mashamba makubwa kupitia program ya Jenga Kesho iliyobora Zaidi (BBT) iliyoanzishwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha maeneo katika wilaya zote yanatengewa miundombinu na kuwapatia wananchi.
Awali akizungumza kwenye mafunzo hayo,Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile ametoa rai kwa vyombo vya Habari kutoa elimu ya kilimo kwa wananchi ili kiwe na tija na kuongeza uzalishaji.
Amesisitiza kuwa idadi kubwa ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma agenda yao kubwa ni kilimo hivyo mafunzo ya kilimo biashara ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki cha serikali ya Awamu ya Sita yenye lengo la kukifanya kilimo kuwa na tija.
Amesema nchi ya Tanzania inalishwa na wakulima wadogo wanaotumia jembe la mkono hivyo amewaasa wakulima wanaopata mafunzo hayo kushiriki kikamilifu ili kupata mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kuzalisha mazao mengi ili kuinua uchumi .
Mafunzo hayo ya kilimo biashara yameandaliwa na Timu ya wataalam kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Kituo cha redio cha Selous FM ya Songea.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.