Wakulima wa korosho mikoa ya Ruvuma ,Lindi na Mtwara wameiomba serikali kuwapelekea pembejeo za korosho za kutosha na kwa wakati ili kuongeza uzalishaji wa zao la korosho ambalo linauzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Wakulima hao kutoka Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ,Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara na Wilaya ya Lindi mkoani Lindi wametoa maombi hayo walipotembelewa kwa nyakati tofauti na Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu.
Khalid Machemba Mkulima wa Namatili Wilaya ya Tunduru amesema kuuza korosho kupitia stakabadhi ghalani ni jambo nzuri isipokuwa changamoto kubwa inayowakabili hivi sasa ni upungufu wa pembejeo za korosho ambazo hazitoshelezi mahitaji ya wakulima hali ambayo amesema inaweza kuchangia kushusha uzalishaji wa zao hilo.
Ally Athuman Mkulima wa Nanyumbu mkoani Mtwara amesema licha ya ukweli kwamba zao la korosho ni dhahabu ya kijani wakulima wanakabiliwa na upungufu wa dawa za kupulizia kwenye mikorosho hali ambayo amesema inayoweza kuathiri zao hilo.
Ally pia ameomba bei ya korosho iongezeke kwa sababu hivi sasa imeshuka na kuathiri wakulima.
Mohamed Juma Mkulima wa Nachunyu Mtama Halmashauri ya Lindi amesema pembejeo za korosho walizopewa msimu huu hazikidhi mahitaji ya wakulima ambao ni wengi na wana mashamba makubwa.
Musa Nura Mkulima wa kijiji cha Malungo Wilaya ya Lindi amesema kijiji chenye wakulima wa korosho 500 kupewa mgawo wa mifuko 100 ya viuatilifu inaleta changamoto kubwa kwa wagawaji hivyo ameiomba serikali kuongeza mgao wa pembejeo ili kuwa na uhakika wa kuongeza uzalishaji wa korosho
Akijibu maombi hayo Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Tanzania Enock Ngalaba amesema serikali inalitegemea zao la korosho kwa ajili ya kukuza uchumi wa wakulima na serikali kwa ujumla hivyo serikali itayafanyia kazi maombi hayo ya wakulima wa zao la korosho ili dawa ziwafikie wakulima kwa wakati.
"Ndiyo maana hata Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini ameamua kufanya ziara ya kuwatembelea ili kuonana uso kwa uso na wakulima wenyewe na kusikiliza kero zinazowakabili",alisema
Amesisitiza kuwa serikali ni sikivu na itachukua hatua haraka kwa sababu uzalishaji wa zao la korosho ukipungua na serikali inapunguza mapato yake na hivyo kurudisha nyuma maendeleo yake.
Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu akizungumzia changamoto ya pembejeo za korosho kwa wakulima wa kusini,amesema kilio cha wengi ni uwepo wa dawa kidogo za kupulizia korosho ambazo hazilingani na mahitaji ya wakulima.
"Wakulima Mimi nimewaelewa kabisa na nawaahidi kuwa nit azungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ili kutatua kero hii kwa wakati"'alisisitiza.
Hata hivyo amesema ana taarifa kuwa serikali ilileta awamu ya kwanza ya dawa hizo na kwamba awamu ya pili pia italetwa ili kuwafikia wakulima.
Ameitaja nia ya serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa kila Mkulima anapata pembejeo za korosho kwa wakati na zinazotosheleza mahitaji ya wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao la korosho ambalo ni dhahabu ya kijani.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Julai 20,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.