wakulima wa ufuta Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ,wamefanikiwa kuvuka lengo la uzalishaji baada ya kuvuna kilo milioni 4,800,997 sawa na ongezeko la asilimia 88.36 zilizowaingizia Sh.bilioni 17.688 ikilinganisha na malengo ya kuzalisha kilo milioni 3,822,561 katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Wakulima hao wameuza ufuta kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos),katika minada saba iliyofanyika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na ongezeko hilo la uzalishaji ni kubwa ikilinganisha na msimu 2022/2023 ambapo walizalisha takribani kilo milioni 2,548,815 zenye thamani ya Sh.bilioni 7.7.
Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro alisema,ongezeko hilo limewezesha wakulima kupata fedha nyingi,hivyo kusaidia kuongeza mzunguko wa uchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa zaidi ya asilimia 43.59 katika kipindi cha mwaka mmoja kupitia zao la ufuta.
“kwa ujumla tumepata mafanikio makubwa kwenye zao la ufuta,kama nilivyosema uzalishaji umeongezeka kwa asilimia 88.36 na kwenye uchumi bei zimeimarika sana,kwa hiyo ukichanganya na ongezeko la uzalishaji utaona kwamba tija iliyoongezeka katika uchumi ni zaidi ya asilimia 43.59”alisema Mtatiro.
Amewaomba wanunuzi,kwenda wilayani humo na kuhakikisha wanashiriki kikamiifu katika ununuzi wa zao hilo ili kuimarisha bei kwa kuwa wilaya hiyo imejipanga kuongeza uzalishaji kufikia kilo milioni 12 katika msimu ujao.
Alisema,suala la kilimo cha ufuta litakuwa ajenda ya kwanza kwenye mikutano yote na wananchi kwa kuwa mpango wa serikali ya wilaya ni kuhakikisha kila mkulima anakuwa na shamba la ufuta.
Mtatiro alisema,hatua hiyo itasaidia sana kupunguza malalamiko na manung’uniko kila inapofika msimu wa kuuza korosho,kwa sababu hawapati fedha za kutosha kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo katika soko la Dunia.
Alisema,wakati Rais Dkt Suluhu Hassan akiendelea kuleta viuatilifu vya bure kwa ajili ya zao la korosho ni vyema wakulima kuwa na mashamba ya mazao mengine ikiwemo ufuta ili kuwaongezea kipato kwenye familia zao.
Kwa upande wake Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu)Iman Kalembo alisema,bei ya ufuta imeongezeka kutoka wastani wa Sh.3,019.80 kwa msimu 2022/2023 hadi Sh.3,661.72 msimu wa 2023/2024 tangu ulipoanza mnada wa kwanza.
Aliongeza kuwa,katika msimu wa mwaka huu wadau wamenufaika kutokana na matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani katika mauzo ya ufuta na wakulima wameendelea kuona uimarikaji wa bei ambao ni muhimu kwa wakulima na serikali kupata takwimu sahihi za mazao yanayozalishwa na ukusanyaji wa mapato yake.
Kalembo,amemshukuru Mkuu wa wilaya kwa kusimamia vema na kutoa ushauri wa mara kwa mara katika uendelezaji wa shughuli za ushirika ambapo amemuomba kuwasimamia na kuwaongoza katika msimu mpya wa kilimo 2023/2024.
Amewahimiza wakulima,kuongeza jitihada za uzalishaji wa zao hilo lililoanza kuonyesha mafanikio makubwa kwao binafsi,vyama vya msingi na serikali kwa ujumla.
Naye makamu mwenyekiti wa Tamcu Pino Chikojola,amewashukuru wakulima,viongozi wa vyama vya msingi(Amcos) na Chama kikuu cha Ushirika kwa kusimamia suala la mauzo ya ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.