Wananchi wa Kijiji cha Kimbanga, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamepata afueni baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa Shilingi milioni 60 kwa ajili ya uchimbaji wa kisima cha maji safi na salama. Hatua hii inalenga kumaliza tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa maji katika kijiji hicho.
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa, Athuman Chola, amesema kuwa Shilingi milioni 300 zimetengwa kwa uchimbaji wa visima vitano wilayani humo, ambapo Kimbanga ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huu.
“Kwa sasa, uchimbaji wa kisima umekamilika na ujenzi wa kioski cha kuchotea maji umefikia zaidi ya asilimia 40. Kazi zinazoendelea ni usambazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, ufungaji wa mashine za kusukuma maji, na uwekaji wa umeme jua ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.”,alisema
Hata hivyo amesema katika vijiji vinne kati ya vitano vilivyopangwa kunufaika na mradi huo, uchimbaji wa visima haujafanikiwa kupata maji chini ya ardhi. Chola amesema RUWASA inatumia mbinu mbadala kama kuboresha chemchem zilizopo na kuanzisha miradi ya mserereko kwa kutumia maji kutoka milimani.
Baadhi ya wakazi wa Kimbanga wameeleza furaha yao kwa hatua hii ya serikali. Adelius Mwingira amesema kuwa mradi wa kisima utawaondolea adha ya kutumia maji yasiyo salama kutoka visima vya asili, huku Bonus Kapinga akisema kuwa kijiji hicho hakijawahi kuwa na maji ya bomba kwa zaidi ya miaka 50.
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini, ikilenga kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.