ZIKIWA zimebaki saa chache kufanyika kwa zoezi la sensa ya watu na makazi,Serikali wilayani Tunduru imekamilisha kwa asilimia mia moja maandalizi yote muhimu ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro, alipokuwa akitoa taarifa ya maandalizi ya sensa kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye yuko kwenye ziara ya kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi katika wilaya zote za mkoa huo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya, jumla ya makarani 1,392 wasimamizi wa tehema 39 na wasimamizi wa mahudhui 141 wamepata mafunzo ya siku kumi na tisa kutoka kwa wakufunzi 53 waliopata mafunzo ngazi ya mkoa.
Alisema,wakati wa maandalizi ya zoezi hilo makarani hao wamepata mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo ikiwamo namna ya kuuliza maswali na kupata taarifa muhimu kutoka kwa wananchi ambao wako tayari kushiriki zoezi hilo ambalo kwa mara ya mwisho limefanyika hapa nchini mwaka 2012.
Mratibu wa sensa mkoa wa Ruvuma Mwantumu Athuman alieleza kuwa,makarani wa sensa watapita kwenye makazi ya wananchi kwa ajili ya kupata taarifa juu ya kaya, hali ya ndoa,walemavu,watoto,elimu na mambo mengine muhimu na kila mwananchi atapaswa kuhesabiwa mara moja tu na sio vinginevyo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas,amewaomba watendaji na watumishi wa serikali kutumia siku chache zilizobaki kwenda kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki sensa ya watu na makazi.
Alisema,katika sensa ya mwaka 2012 wilaya ya Tunduru haikufanya vizuri kutokana na baadhi ya wananchi kukataa kuhesabiwa kutokana na upotoshaji wa baadhi ya watu kuingiza zoezi hilo na imani ya dini.
Alisema,matokeo yake serikali ilishindwa kupata idadi kamili ya wananchi wake na hivyo kushindwa takwimu na taarifa sahihi ambazo zingesaidia wilaya hiyo kuwa na sifa ya kupata Halmashauri ya pili.
“kama wananchi hawatajitokeza kwa wingi na kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa sensa,basi itakuwa vigumu kwa serikali kufikiria kuwapa Halmashauri nyingine”alisema Kanali Laban.
Aidha,amewaagiza viongozi wa wilaya hiyo kwenda kusimamia na kuratibu vizuri mchakato wa kusajili majina ya wakulima wenye sifa ya kupata mbolea ya ruzuku na kuonya kuwa,mwananchi au kiongozi atakayekwenda kinyume na zoezi hilo atachukuliwa hatua.
“ni marufuku kwa mwananchi au kiongozi kuuza mbolea hiyo,nawaomba sana endeleeni kuhamasisha wakulima kujiandikisha kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku ili iweze kuongeza uzalishaji mashambani”alisisitiza Kanali Laban.
Alisema,zoezi hilo halihitaji kutoa fedha wala rushwa ya aina yoyote ni zoezi la bure na kuwaomba viongozi wa ngazi mbalimbali katika wilaya hiyo kwenda kusimamia utekelezaji wake.
Kanali Laban alisema kuwa,kama zoezi hilo litasimamiwa vizuri mkoa wa Ruvuma utaendelea kuwa wa kwanza katika uzalishaji na hata kaya maskini zinazopokea ruzuku kupitia Tasaf zitapungua.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Said Bwanali alisema,wananchi na watumishi wa wilaya hiyo hawana shaka juu ya utendaji wake.
Bwanali,amempongeza Kanali Labani kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ambapo amehaidi kuwa Halmashauri hiyo itampa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake ikiwamo kushiriki na kusimamia vyema zoezi la sensa ya watu na makazi
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.