Wananchi wa Kijiji cha Litumbandyosi kilichopo Kata ya Litumbandyosi, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kijijini hapo, ambapo Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga anatarajia kuwasha umeme kesho Oktoba 8, 2023.
Pongezi hizo zimetolewa leo Oktoba 7, 2023 wakati wa mahojiano maalum na wananchi wa kijijini hicho, namna walivyopokea ujio wa umeme, changamoto walizokuwa wakipitia kutokana na kukosa umeme pamoja na fursa watakazoenda kuziibua kutokana na ujio wa umeme wa REA.
“Tunampongeza Mhe. Rais kwa kutuletea umeme, tumekuwa tukiona umeme kwenye miji mikubwa, hatukuwahi kufikiria siku moja na sisi kijiji chetu kitakuja kuwa na umeme. Tunashukuru kesho Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga anatuwashia umeme hapa kijijini,” amesema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Litumbandyosi, Mikael Mwingira.
Ameendelea kusema kuwa, umeme huo utafungua fursa mbalimbali kijijini hapo ikiwemo uanzishwaji wa mashine za kusaga za umeme, tofauti na mashine za mafuta ambazo wamekuwa wakizitumia. Vilevile amesema kuwa, ujio wa umeme kijijini hapo utawezesha uanzishwaji wa mashine za kubangulia korosho, ambazo zilikuwa hazipo kijijini hapo, kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika.
Naye Diwani wa Kata wa Litumbandyosi, Mhe. Prisca Haule amesema walikuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa viwanda kijijini hapo, licha ya kuwa ni wazalishaji wakubwa wa korosho na mpunga. Hivyo kufika kwa umeme wa REA kutawezesha kuanzishwa viwanda mbalimbali vikiwemo vya kubangua korosho na kukoboa mpunga.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa vinywaji kijijini hapo, Elbert Kinunda amesema walikuwa wakipata changamoto mbalimbali katika kutumia umeme wa sola, ikiwemo kipindi cha mvua, ambapo betri zinashindwa kujichaji kutokana na kukosekana kwa jua, hivyo biashara katika mazingira magumu ya kukosa mwanga wakati wa usiku.
“Baada ya kuwashiwa umeme wa REA nina amini maendeleo yatakuwa makubwa sana, hata sisi wafanyabiashara wa vinywaji tutaanza kuuza vinywaji vya baridi. Umeme pia utatuwezesha kuanzisha viwanda vya kuchomea vyuma, ambayo tulikuwa tunashindwa kuvianzisha kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika,” amesema Kinunda. Wampongeza Rais Samia Kufikiwa Umeme wa REA
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.