WAKAZI wa Kata ya Masonya Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha kujenga barabara ya Tunduru-Masonya-Nambalapi yenye urefu wa kilomita 6 ambayo ilikuwa ni changamoto kwa wakazi hao.
Wametoa shukurani hizo jana mbele ya Diwani wa kata ya Masonya Said Bwanali ,wakati wa ziara yake ya kukagua matengenezo ya mradi wa barabara hiyo yanayofanyika kutoka kiwango cha udongo na kwenda kiwango cha changarawe na kusimamiwa na wakala wa barabara za mjini na vijijini Tanzania (Tarura)wilaya ya Tunduru.
Habibu Ali mkazi wa kijiji cha Masonya alisema,changamoto kubwa ya barabara hiyo ilikuwa wanapohitaji kwenda Tunduru mjini kufuata huduma mbalimbali za kijamii hakukuwa na usafiri wa uhakika kutokana na ubovu na hapakuwa na barabara nyingine mbadala.
Habibu ambaye ni dereva wa Bajaji inayofanya safari kati ya Tunduru mjini na kijiji cha Masonya alisema,barabara hiyo iliyowapa wakati mgumu hasa wanapohitaji kufika Tunduru mjini kufuata huduma za kijamii au kusafirisha wagonjwa ambapo ameipongeza serikali kwa kuipatia fedha Tarura ziliwezesha kufanya matengenezo ya barabara hiyo.
Alisema,hata walipotaka kusafirisha vifaa vya ujenzi ilikuwa kero kubwa maana walilazimika kutumia watu kubeba na kufikisha sehemu husika hali iliyosababisha gharama za maisha kuwa juu.Cheva Saleh aisema kuwa,hali ilikuwa mbaya zaidi hasa nyakati za masika kutokana na utelezi uliokuwepo ambapo walilazimika kutembea kwa miguu au kupanda baiskeli, jambo lililochelewesha sana maendeleo ya wananchi wa Masonya.
Diwani wa kata ya Masonya Said Bwanali,amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya katika kuharakisha maendeleo ya wananchi na ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Bwanali ambaye ni makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru alisema,katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa Dkt Samia kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo nan chi kwa ujumla.
Ametaja baadhi ya mafanikio hayo ni kuimarika kwa huduma za afya,maji na barabara na kwa mara ya kwanza tangu Uhuru wa Tanganyika na sasa Tanzania kata hiyo imepata barabara bora na imara iliyojengwa kwa changarawe inayopitika majira yote ya mwaka.
Alisema,kata ya Masonya ni ya kilimo hivyo sehemu kubwa ya wakazi wake ni wakulima ambapo awali walishindwa kusafirisha mazao kwenda sokoni kutokana na miundombinu mibovu ya barabara na kuwapongeza watendaji wa Tarura kwa kusimamia vuzuri matengenezo ya barabara hiyo.
Kwa upande wake kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Msolwa Julius alieleza kuwa,mradi huo unajumuisha ujenzi wa barabara tatu za Marumba-Mbesa kilomita 12,Kangomba-Marumba-Njenga kilomita 24 na Tunduru-Masonya-Nambalapi kilomita 6.
Alisema,gharama za mradi huo ni shilingi milioni 650 na katika kipande cha Tunduru-Masonya kazi iliyofanyika ni kufungua barabara hiyo na kuweka kifusi umbali wa km zote 6 na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wameanza kuitumia barabara hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.