Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amewataka wananchi wa Tanzania kuzingatia Elimu inayotolewa kupitia kampeni mbalimbali ili kuachana na mila zinazoweza kuwa vichocheo vya maambukizi ya VVU.
Ametoa rai hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa imefanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
"Ninaendelea kutoa rai kwa watanzania kuzingatia maudhui ya Elimu inayotolewa kupitia kampeni mbalimbali, kuachana na mila zinazoweza kuwa vichocheo vya maambukizi na kuendelea kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI," alisema Mhe. Dkt. Mpango.
Ameongeza kuwa kundi la vijana hasa wa kike wapo kwenye hatari zaidi ya kupata VVU, hivyo ameiagiza Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kushirikiana na wadau na jamii kwa ujumla kuweka mkazo katika kudhibiti mazingira yanayochochea maambukizi.
Kupitia maadhimisho hayo ametoa wito kwa vijana kujitambua, kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya VVU, na ambao wanaishi na maambukizi kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi kwa usahihi na kuimarisha afya zao.
Kwa upande mwingine Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya mwaka huu ambayo inasema Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI inakumbusha umuhimu wa kuwa na mikakati na mbinu bora za kuendelea kushirikisha jamii ili kufikia malengo ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi ya VVU ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo amesema kuwa maadhimisho hayo mwaka huu yanatoa msisitizo kwa vijana kuendesha mijadala na kuwa na matukio mbalimbali ili kuwawezesha kupata Elimu kwa pamoja kuhusiana na masuala ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Naye Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amesisitiza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kuongeza jitihada kuhakikisha inafanya mapitio ya kisera, mikakati na miongozo ya kutoa huduma bora kwa jamii katika afua zote za mwitikio dhidi ya VVU na UKIMWI.
Amesisitiza kwamba UKIMWI bado upo, hivyo Taifa lina kila sababu ya kuendelea kuzuia maambukizi mapya na kuhakikisha walio na maambukizi wanafubaza VVU.
Siku ya UKIMWI Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 1 Desemba ambayo inalenga kueneza ufahamu kuhusu UKIMWI, kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI, kuhamasisha hatua za kuzuia maambukizi mapya, na kupambana na unyanyapaa unaohusiana na VVU au UKIMWI.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.