WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kata ya Amani Makolo Halmashauri ya wilaya Mbinga,wametakiwa kutumia kiasi cha fedha wanazopata kuwekeza katika elimu ya watoto wao kwa kuwapeleka shule, badala ya kuzitumia katika anasa.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,wakati akizungumza na wanufaika wa mpango huo wa kata ya Amani Makolo Halmashauri ya wilayani Mbinga akiwa katika ziara ya siku moja kutembelea kaya maskini zinazopokea ruzuku ya fedha kutoka mfuko wa maendeleo ya jamii(Tasaf).
Alisema, madhumuni ya mpango kunusuru kaya maskini ni kuziwezesha jamii hasa kaya hizo kuongeza kipato,fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji ya msingi ikiwamo chakula,malazi,afya, elimu na kuziwezesha kuwekeza kwenye rasilimali watu kwa kuwapa ruzuku yenye masharti kwa watoto kuhudhuria shule na kliniki.
Ibuge amewataka walengwa hao, kutumia fedha hizo kama ilivyo mpango wa Serikali ambao unalenga kuhakikisha kila mtoto hapa nchini anayetoka katika familia maskini anapata elimu,matibabu kwa wazazi na walezi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na wanufaika kujikimu kimaisha.
Alisema, ni muhimu kutambua uzito wa kile wanachopokea na Serikali ambayo ina nia njema na wananchi kwa kutafuta na kutoa fedha ili ziweze kubadili maisha ya baadhi ya watu wenye kipato duni ili kuwajengea uwezo kiuchumi na kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo katika jamii.
Alisema, unufaikaje huo ni lulu na hauwezi kuendelea milele, hivyo amewakumbusha wanufaika wa mpango huo kukumbuka kujiwekea akiba na kuanzisha miradi ya kiuchumi ili waweze kujitegemea siku za baadaye badala ya kuendelea kuitegemea Serikali.
Aidha Jenerali Ibuge,amewataka wananchi wa wilaya ya Mbinga kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji wakati huu ambao wanaendelea na shughuli zao za kilimo na kuwaagiza viongozi wa vijiji,kata na wilaya kusimamia sheria za mazingira zilizopo.
Amewapongeza baadhi ya wananchi waliojiunga na mfuko wa afya ya jamii,hata hivyo amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuhamasisha watu wengine kujiunga na mfuko huo ili waweze kupata matibabu kwa urahisi pindi wanapougua.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo alisema, wilaya hiyo yenye Halmashauri mbili imepokea jumla ya Sh.3,122,582,400.00 kwa ajili ya malipo ya walengwa 12,067 wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika vijiji 195.
Alisema,Halmashauri ya wilaya imepokea Sh.2,243,912,400.00 kwa ajili ya malipo ya kaya 8,669 na Halmashauri ya Mji Mbinga imepokea Sh.878,670,000.00 kwa ajili ya kaya 3,398.
Mamgosongo alimueleza Mkuu wa mkoa kuwa, mwaka wa fedha 2020/2021 malipo yamefanyika katika awamu sita na kaya 8669 zimenufika kwa vipindi vya miezi miwili katika kila dirisha la malipo kwa kupokea ruzuku ya msingi na ruzuku ya masharti na Sh.2,243,912,400.00 zimelipwa kwa kaya maskini.
Alisema,kupitia mpango huo kumekuwa na mafanikio makubwa ambapo fedha zinazohawilishwa kwa kaya za walengwa vijijini zimeweza kutoa msukumo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na ongezeko la mzunguko wa fedha.
Mangosongo alitaja mafanikio mengine ni baadhi ya kaya kutumia sehemu ya fedha wanazopata kujiunga na mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa ambapo jumla ya kaya za walengwa 4,918 kati ya kaya 8,669 sawa na asilimia 77 zimejiunga na mfuko huo.
Alisema, kupitia mpango huo kasi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kupelekwa kliniki ni kubwa na mahudhurio ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari yameongezeka kufuatia kuboreka kwa maisha ya watoto wanaotoka katika kaya maskini.
Mwisho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.