Na Albano Midelo,Dodoma
WATAALAM 180 kutoka Sekretarieti za mikoa 26 Tanzania Bara wameanza mafunzo ya siku tano kuhusu mfumo mpya wa ununuzi wa umma (NeST).
Mafunzo hayo yanayofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma yameandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi ya Umma (PPRA).
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa PPRA Joakim Maswi amesema PPRA imeunda mfumo mpya wa ununuzi wa umma unaoitwa National eprocurement Sytem of Tanzania (NeST) ambao umeanza kutumika Julai Mosi 2023.
Amesema serikali imepitisha sheria ya kuanza kutumika mfumo mpya wa ununuzi wa umma NeST baada ya kubaini changamoto za kiufundi zilizojitokeza kwenye mfumo wa ununuzi wa awali (TANePS) na lengo ni kuhakikisha hadi Agosti 15,2023 Taasisi zote zianze kutumia mfumo wa NeST.
“Mfumo wa TANePS utakoma kutumika ifikapo tarehe 30 Septemba 2023,kwa hiyo mara baada ya mafunzo haya,ninyi RS zote 26 ambao mmefika hapa Dodoma mtakwenda kuwa walimu wa mfumo mpya wa ununuzi NeST katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara’’,alisema Maswi.
Amezitaja faida za mfumo mpya wa ununuzi wa umma kuwa ni Pamoja na kuongeza wigo wa ushiriki kwenye ununuzi,uwajibikaji,kupunguza muda wa mchakato,upatikanaji wa taarifa na kupunguza mianya ya rushwa.
Faida nyingine amezitaja kuwa ni uandaaji wa zabuni zote na uombaji wa zabuni utafanyika ndani ya mfumo,wazabuni watajisajiri na kupandisha nyaraka zao zote kwa mara moja na nyaraka zote zitasainiwa ndani ya mfumo.
Akuzungumza wakati anafungua mafunzo hayo,mgeni rasmi Katibu Mkuu wa TAMISEMI Adolf Ndunguru amesema wataalamu ngazi ya mikoa baada ya kuhitimu mafunzo hayo wanakwenda kuwa walimu kwa watumiaji wengine wa mfumo wa NeST .
Amesema sekta ya ununuzi wa umma inachukua takriban asilimia 70 ya Bajeti ya Serikali hivyo amesisitiza kuwa ununuzi wa umma ni eneo nyeti hali iliyosababisha serikali kutenga fedha nyingi ili kufanikisha malengo na matarajia ya nchi kwenye ununuzi.
Ameutaja uamuzi wa serikali kuamua kuanza kutumia mfumo wa NeST ni kuingia katika mapambano ya adui rushwa ambaye ameshamiri kwenye mfumo wa ununuzi wa umma na kwamba mfumo utaongeza uwajibikaji kwa watendaji hasa PPRA wanaosimamia mfumo wa ununuzi wa umma.
“Mfumo huu umepewa uwezo wa kufuatilia mienendo yote ya ununuzi kwenye Taasisi za umma,hata ikitokea kumefanyika uzembe,ni rahisi kumtambua mtu aliyefanya uzembe huo,natoa wito kwa wote wanaohusika kwenye mfumo wa ununuzi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili,sheria na taratibu zote’’,alisisitiza Ndunguru.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo amepongeza ujasiri wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuridhia mfumo mkubwa wa ununuzi wa umma wenye maslahi mapana kwa Taifa letu kujengwa na wataalam wa hapa nchini hivyo kuepuka wataalam wa nje.
Mfumo wa NeST utakuwa mbadala wa mfumo unaotumika hivi sasa wa TANePS,unatarajiwa kutatua changamoto za kiufundi na hivyo kukidhi mahitaji ya Serikali Katika Sekta ya ununuzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.