WAKAZI zaidi ya 2900 wa kijiji cha Mbangamao Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wanatarajia kunufaika na mradi wa maji unaogharimu shilingi bilioni 1.8.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Meneja RUWASA Wilaya ya Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkala amesema mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 65 unatarajia kukamilika Januari 2023.
Hata hivyo amesema mradi umechelewa kukamilika kutokana na Mkandarasi wake kuongezewa muda wa utekelezaji kutoka miezi sita hadi tisa.
“Hadi sasa ujenzi wa chanzo umekamilika kwa asilimia 100,ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la lita 200,000 umefikia asilimia 95 na uchimbaji mtandao wa maji umefikia umbali wa kilometa 14”,alisema.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amewaagiza watumishi wa RUWASA kuanza kujenga vituo vya kuchotea maji kwa sababu tayari maji yapo ndani ya tanki la mradi.
Amesema wananchi wanahitaji maji hivyo RUWASA isisubiri uzinduzi wa mradi utakapokamilika badala yake waanze kuwasambazia maji wananchi wa Mbangamao. “Kwenye miradi ya maji ya mserereko unapokuwa umejenga tanki unatakiwa uanze kuwanywesha maji wananchi “,alisema.
Amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kuteseka kwa sababu maji ni bidhaa muhimu katika maisha ya kila siku.
Naye Joseph Kapinga Mkazi wa kijiji cha Mbangamao amesema wanamshukuru Rais Samia kwa mradi wa maji ambao unakwenda kumaliza kero ya kusafiri umbali mrefu kwa akinamama na watoto kutafuta maji.
Mradi wa maji Mbangamao ni miongoni mwa miradi nane ya maji katika Wilaya ya Mbinga inayotekelezwa na RUWASA kwa fedha za mfuko wa maji na serikali kuu.
Imeandikwa na Albano Midelo,Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.