WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) waliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wanamiliki hekta zaidi ya laki moja kwa ajili ya mashamba ya miti ya kupanda.
Kati ya hekta hizo,hifadhi ya shamba la miti Wino ina ukubwa wa hekta 39,718,shamba la miti Mpepo lina ukubwa wa hekta 20,905 na shamba jipya la miti la Tunduru lina ukubwa wa hekta 50,000.
Akizungumzia hifadhi ya shamba la miti Wino Halmashauri ya Madaba Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo Glory Kasmiri amesema hifadhi ya msitu wa Wino ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na TFS.
Hata hivyo amesema hifadhi hiyo hivi sasa ina ukubwa wa hekta 39,781 zinazoundwa katika safu tatu katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea ambazo ni safu ya Wino yenye hekta 2,259,safu ya Ifinga yenye hekta 29,000 na safu ya Mkongotema yenye hekta 8459.
Ameitaja hifadhi ya msitu ya Wino ilianza kuendelezwa na TFS mwaka 2010 ikihusisha eneo dogo la msitu wa asili wenye ukubwa wa hekta 2259.
Mhifadhi Kasmir amesema kati ya mwaka 2014 na 2016 hifadhi ilipata maeneo katika vijiji vya Ifinga na Mkongotema ambapo hadi sasa jumla ya hekta 5,495 zimepandwa miti ya aina mbalimbali sehemu kubwa ikiwa ni miti jamii ya misindano.
“Shamba la miti Wino limeendelea kuboresha mahusiano na wananchi,pia TFS kupitia shamba la miti Wino tumefadhili mradi wa maji kwa wananchi wa Kijiji cha Ifinga uliogharimu shilingi milioni 482’’,alisema Mhifadhi Kasmiri.
Licha ya changamoto ya baadhi ya wananchi kuanzisha moto maeneo hatarishi kwenye hifadhi wakati wa uandaaji wa mashamba,Kasmir amesema shamba la miti Wino limepata mafanikio mbalimbali yakiwemo kuimarika uhifadhi wa eneo la hifadhi na shamba linatoa ajira za muda mrefu na mfupi ambapo watu 4000 kila mwaka.
Amesema uwepo wa shamba la miti Wino umevutia wawekezaji wengine ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambacho kimepewa ardhi na Kijiji cha Ifinga yenye ukubwa wa hekta 10,000 kwa ajili ya kupanda miti.
Licha ya uwepo wa shamba la miti Wino,Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania pia wanamiliki shamba la miti Mpepo ambalo lilianzishwa mwaka 2018 likiwa na ukubwa wa hekta 2017 ambapo hadi sasa zimefikia jumla ya hekta 3905 katika wilaya ya Nyasa pekee.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Mpepo John Kimolo amelitaja eneo la shamba la Mpepo hivi sasa lina ukubwa wa takriban hekta 20,905 ambalo linapita katika wilaya za Nyasa,Songea na Namtumbo.
Hata hivyo amesema Shamba la Mpepo kupitia TFS limefanikiwa kupata eneo lenye jumla ya hekta 50,000 katika wilaya ya Tunduru kwa ajili ya kuanzisha shamba jipya la miti ambapo serikali katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 imetenga bajeti ya kuanza kupanda miti katika shamba la hekta 100.
“Katika shamba la miti Mpepo hadi sasa imepandwa miti hekta 2240 ,hekta 1440 imepandwa miti jamii ya misindano (Pines) katika tarafa ya Mpepo na Liwilikitesa wilaya ya Mbinga na hekta 400 imepandwa miti jamii ya misaji (Teaks) katika hifadhi ya Kipiki wilaya ya Namtumbo na hekta 400 za za misaji zimepandwa eneo la Liuli wilaya ya Nyasa’’,alisema Kimolo.
Mhifadhi Mkuu huyo amezitaja baadhi ya faida za kuanzishwa kwa shamba la miti Mpeo kuwa ni chanzo cha mapato serikalini,kutoa ajira za muda 3000 kwa wananchi kwa mwaka,upatikanaji wa malighafi wa viwanda vya mbao na kuboresha mazingira.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ni miongoni mwa wadau muhimu hapa nchini katika suala nzima la uhifadhi endelevu na utunzaji wa mazingira.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Desemba 21,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.