WAFANYAKAZI mkoani Ruvuma wamelalamikia mishahara yao kuwa bado ni midogo ukilinganisha na hali halisi ya maisha ya wafanyakazi.
Akisoma risala ya wafanyakazi wa Mkoa wa Ruvuma katika sherehe ya Mei Mosi iliyofanyika kimkoa mjini Mbambabay wilayani Nyasa,Katibu wa TUGHE Mkoa wa Ruvuma Ismail Mudathir amesema katika sekta ya umma na binafsi mishahara haikidhi mahitaji ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha.
“Tunaiomba serikali kupitia Mei Mosi hii,kwa itutazame jicho la kipekee kabisa iongeze mishahara na kuboresha maslahi kwa wafanyakazi kwa sababu ni muda mrefu sana mishahara haijaongezwa’’,alisisitiza Katibu wa TUGHE.Amesema watumishi wa Mkoa wa Ruvuma,wanakabiliwa na changamoto za kiutumishi zikiwemo baadhi ya waajiri kutowatendea haki baadhi ya watumishi hali ambayo ina punguza molali kwa wafanyakazi.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kutolipwa madeni ya uhamisho wa watumishi,baadhi ya watumishi kutopandishwa madaraja kwa wakati na baadhi ya waajiri kutolipa nauli za watumishi na mizigo yao wanapostaafu.
Hata hivyo licha ya changamoto hizo Katibu huyo wa TUGHE kwa niaba ya watumishi mkoani Ruvuma amesema,wafanyakazi wanaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi mapana ya nchi ya Tanzania.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba ametoa rai kwa watumishi kuwa na subira kwa sababu serikali ya Awamu ya sita imedhamiria kuboresha maslahi ya watumishi.
“Serikali mwezi huu imeanza kutoa barua za kuwapandisha madaraja watumishi wa umma wanaostahili katika nchi nzima na katika Halmashauri za wilaya baadhi ya watumishi wameanza kupata barua za kupandishwa madaraja kupitia maafisa utumishi’’,alisema Chilumba.
Hata hivyo amewaagiza waajiri kuhakikisha wanawalipa mafao na haki zao zote watumishi wanaostaafu na kuwaagiza waajiri kwenye Halmashauri na Taasisi zote za serikali kuacha kuchelewesha fedha za malipo ya likizo kwa watumishi wanaokwenda likizo.
Mei Mosi ni siku ya wafanyakazi wote duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei Mosi,kauli mbiu ya mwaka huu ni maslahi bora,mishahara juu,kazi iendelee.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Tarehe 2/5/2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.