WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Ajira na Watu wenye ulemavu Jenista Mhagama(Mb) amezindua huduma ya masta boda iliyoratibiwa na Benki ya NMB.
Kwa mara ya kwanza kampeni hii ilizinduliwa Oktoba 2019 jijini Dar es salaam na kufuatiwa Mkoa wa Pwani na sasa Mkoa wa Ruvuma.
Uzinduzi huo wa kampeni hiyo umefanyika kwenye ukumbi wa Misheni Peramiho nje kidogo ya Mji wa Songea,lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa vijana wanaendesha pikipiki wanaingizwa katika mfumo rasmi wa kifedha kupitia benki ya NMB.
Akizungumza kabla ya kuzindua kampeni hiyo Waziri Mhagama amewataka vijana kuunga mkono dhamira ya kujiunga na masta boda ambayo inaweza kuleta mabadiliko ya kiumfumo katika sekta ya bodaboda iliyoajiri vijana wengi.
Amesema asilimia 56 ya nguvukazi nchini ni vijana na kwamba ajira rasmi hivi sasa ni chache na kwamba vijana wanaweza kutafuta mifumo tofauti ya ajira na kujiajiri au kusaidiwa kutengeneza ajira.
“Leo hii Benki ya NMB inataka kubadilisha mfumo wa ajira ya masta boda kwenda kuwa ni ajira rasmi iliyorasmishwa na kuwa ajira yenye staa miongoni mwa ajira nyingine zinazopatikana Tanzania’’,alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB Makao makuu Benedikto Baragomwa amesema huduma ya mastaboda itawawezesha vijana kuwa na mfumo rahisi wa malipo ya huduma za bodaboda.
Amesema huduma sasa itawaweka bodaboda katika mfumo rasmi wa kifedha kupitia benki ya NMB na kwamba benki hiyo inatarajia kuwafikia waendesha bodboda zaidi ya 75,000 katika nchi nzima.
Amesema idadi kubwa ya waendesha pikipiki tayari wamefungua akaunti na kwamba NMB inatarajia kuwafikia bodaboda 2000 wilayani Songea kutoa mikopo ya bodaboda na bajaji kwa vijana 160.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo,katika nchi nzima kuna waendesha pikipiki zaidi ya milioni mbili ambao bado hawajaingia kwenye mfumo wa kibenki hivyo amesema NMB inatoa fursa ya vijana hao kuingia katika mfumo rasmi wa kifedha.
Naye Ofisa wa NMB Kitengo cha Mastakadi Filbert Kazimili akizungumza katika uzunduzi huo amesema biashara ya pikpiki ilianzia mkoani Ruvuma mwaka 2004 ambapo amesema masta boda ni njia nyepesi ya kupokea malipo kwa njia ya simu.
“Benki ya NMB imeshirikiana na masta kadi kuhakikisha kwamba madereva wa bodboda wanapokea malipo kwa njia salama na uhakika kupitia mtandao’’,alisema.
Kwa mujibu wa Kazimili,kwa muda mrefu wamekuwa wanaangaika na ajira na kwamba sekta ya bodboda imekuwa moja ya sekta zinazotengeneza ajira kwa vijana na kwamba NMB imeamua kutoa fursa za kibenki kwa vijana kupitia boda masta boda.
Amesema NMB imekusudia vijana waweze kuaminika na kukopeshwa na kwamba kwa kuanzia kila kijana anayefanya kazi ya bodboda atafungua akaunti ya benki ili akipokea malipo kupitia boda masta ambapo pesa inaingia moja kwa moja kwenye akaunti yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodaboda mkoani Ruvuma Hamisi Hassan Maulid amesema huduma ya usafirishaji ilianza mwaka 2004 katika Manispaa ya Songea kukiwa na wasafirishaji wachache ambapo hadi kufikia mwaka 2008 idadi kubwa ya vijana waliokuwa wanakosa ajira waliamua kujiingiza kwenye huduma hiyo.
Kiongozi huyo wa bodbado ambaye amehitimu chuo kikuu na kukosa ajira rasmi amesema hadi kufikia mwaka 2019 idadi ya madereva bodaboda katika Mkoa wa Ruvuma ilifikia 85,000.
Anayataja mafanikio ambayo madereva boda wameyapata hadi sasa kuwa ni kupata kipato,kusomesha watoto,ujenzi wa nyumba za makazi na kwamba kazi hiyo ni ajira mbadala ambayo imepunguza kasi ya vijana kushinda vijiweni.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema ameipongeza NMB kwa kuanzisha huduma hiyo ambapo amewaomba waendesha bodaboda kujiunga na huduma hiyo sanjari na kuchukua vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo vitawawezesha kupata mikopo kupitia NMB.
“Nawaomba vijana wa bodboda tujiunge,tutambuane kwa sababu kuna manufaa makubwa ya kiuchumi na kiusalama endapo mtajiunga na huduma ya boda masta’’,alisisiza.
Uchunguzi umebaini kuwa dereva wa boda boda kwa siku anapofanyakazi vizuri anaweza kuingiza kipato cha kati ya shilingi 200,000 hadi 300,000 ambao ni mshahara anaolipwa mtumishi anayefanyakazi mwezi mzima.
Ameshauri waendesha pikipiki wote kujiunga na mfumo wa masta boda kwa sababu utasaidia kujenga tabia ya kutunza akiba na kuleta mabadiliko chanya katika maisha.
Mfumo wa masta boda utamwezesha dereva wa pikipiki kupata malipo moja kwa moja kutoka kwa mteja hali ambayo itasaidia fedha zake kuwa salama kwenye akaunti na kupandisha hadhi ya biashara.
Mwandishi ni Mchangiaji wa gazeti hili,mawasiliano yake ni baruapepe albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.