WAZIRI wa Mipango na Uwekezaji Prof.Kitila Mkumbo ameshangazwa na uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo ambapo katika Halmashauri ya Madaba na Songea mkoani Ruvuma wawekezaji toka nje wamewekeza katika mashamba yenye ukubwa wa hekta zaidi ya 2500.
Akiwa katika Halmashauri ya Madaba,Waziri Mkumbo alishuhudia uwekezaji mkubwa wa Kampuni ya kigeni ya Silver Ndolela iliyowekeza katika shamba lenye ukubwa wa hekta 1500 ambapo kampuni hiyo inazalisha mbegu za aina nne kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji.
Meneja wa shamba hilo alizitaja mbegu zinazozalishwa na Kampuni hiyo kuwa ni maharagwe,mahindi,ngano na viazi ambapo Waziri Mkumbo alisisitiza uwekezaji katika mbegu bora ni muhimu hapa nchini kwa kuwa moja ya changamoto katika kilimo ni upatikanaji wa mbegu bora.
“Wakulima wetu wanatumia mbegu hafifu wanalima eneo kubwa na kupata mavuno kidogo,hivyo uwepo wa shamba hili la mbegu bora itasaidia kuboresha kilimo hapa nchini ’’,alisisitiza Waziri Mkumbo.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji pia alikagua shamba kubwa la kilimo cha umwagiliaji la Kampuni ya AVIV katika Kijiji cha Lipokela Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Prof.Mkumbo amefurahishwa na uwekezaji mkubwa katika shamba kahawa uliofanywa na Kampuni ya AVIV TANZANIA LTD ambapo Kampuni hiyo inalima na kuchakata kahawa kwa mwaka tani zaidi ya 2000 katika shamba la kahawa lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 1000.
Waziri Mkumbo amesisitiza kuwa kulima na kuchakata kahawa ni uwekezaji mkubwa ambao umefanywa kwa kuwezeshwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) ambapo amesema uwekezaji huo unashughulikia sekta ya kilimo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Ameipongeza Kampuni ya AVIV kwa kutekeleza mambo matatu kwa wakati mmoja ikiwemo kilimo cha kahawa,kuchakata mazao ya kilimo hivyo kutoa ajira kwa watanzania na kuongeza mauzo nje ya nchi.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Kapenjama Ndile akizungumza baada ya Waziri kutembelea maeneo ya uwekezaji katika shamba la Madaba na Lipokela,ameutaja Mkoa wa Ruvuma kwa miaka 13 sasa unaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Amesema katika kutambua mchango wa Mkoa wa Ruvuma kwenye uzalishaji chakula ,mwaka huu kwenye maadhimisho ya Nanenane Kitaifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan alitoa chetu maalum kwa Mkoa wa Ruvuma kwa kushika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji nafaka.
Awali akitoa taarifa ya Kampuni ya AVIV, Meneja Msaidizi wa Kampuni ya AVIV TANZANIA Muthana Namb amesema asilimia 80 ya kahawa inayochakatwa na Kampuni hiyo inauzwa katika nchi mbalimbali Duniani zikiwemo Marekani,Saudi Arabia,India, Japan, Jordan na Afrika ya Kusini.
Naye Mwakilishi wa Kampuni hiyo anayesimamia kilimo Johson Kishumba amesema Kampuni ya AVIV TANZANIA imekuwa kampuni ya kwanza katika bara la Afrika kupewa Tuzo ya Water Stewardship inayotolewa na SGS ya nchini Afrika ya Kusini kwa kufanya vizuri kwenye kilimo na mazingira.
Hata hivyo amesema kampuni hiyo inashirikiana na wananchi wanaozunguka shamba hilo ambao wamekuwa wanasaidiwa katika sekta za afya,maji na mazingira na kwamba baadhi ya wananchi wanapata ajira kwenye shamba la kahawa.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Ruvuma kwa lengo la kukutana na wawekezaji,kusikiliza mafanikio na changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi hatimaye kuimarisha zaidi eneo la uwekezaji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.