Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wanaojenga Shule ya sekondari ya wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa ili waanze kupokea wanafunzi.
Ametoa agizo hilo, Januari 6, 2023 mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo inayotarajia kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2023.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike kwa kujenga shule za wasichana kwenye mikoa yote ili kumpunguzia mtoto wa kike changamoto zilizokuwa zikimkabili. “Si kwamba amemtenga mtoto wa kiume hapana, ameamua kwenda nao wote.”
Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 4 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), awamu ya kwanza ilianza April 2022 na inatarajiwa kukamilika Januari 30, 2023 na kugharimu shilingi bilioni tatu. Shule hiyo itakapokamilila itapokea wanafunzi 1,080 ambapo awamu ya kwanza itapokea wanafunzi 600.
Awamu ya kwanza imehusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mabweni matano, bwalo, vyumba 12 vya madarasa, jengo la utawala, nyumba ya mwalimu, mfumo wa maji safi na maji taka, vyoo matundu 16, uzio, kichomea taka, chumba cha jenereta na njia za kutembelea.
Pia, awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni moja itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu tatu, chumba cha ICT, Maktaba, nyumba nne za walimu na mabweni manne.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.