Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha inajenga na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo yote yasiyofikika ili kusaidia wananchi kupata huduma za kijamii, kibiashara na uwekezaji.
Waziri Bashungwa amesema hayo mkoani Ruvuma Januari 26, 2024 wakati akiwa ziarani kukagua miundombinu ya barabara kutokea Songea mjini hadi wilayani Nyasa kupitia barabara ya Likuyufusi - Mtomoni yenye urefu wa Kilometa 124 inayotarajia kujengwa kwenye kipande cha kwanza cha Likuyufusi - Mkayukayu chenye urefu wa Kilometa 60 kwa kiwango cha lami pamoja na kukagua maeneo ambapo madaraja ya Mkenda na Mitomoni yatakapojengwa.
“Niwatake wasaidizi wangu, ninapokuwa katika ziara mikoani sitaki nikague barabara zilizojengwa kwa lami, nataka nikague maeneo ambayo hayana miundombinu ili Serikali ione namna ya kujipanga kutatua changamoto za wananchi”, amesisitiza Bashungwa.
Baada ya kukagua maeneo hayo, Waziri Bashungwa ametoa miezi miwili kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa daraja la zege katika eneo la Mitomoni ili wananchi wa maeneo hayo waondokane na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.
Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaunganishwa na barabara ya Unyoni Mpapa - Liparamba - Mkenda pamoja na barabara ya Likuyufusi - Mkenda kupitia Mto Ruvuma.
“Ujenzi wa Daraja hili utaunganisha Wilaya ya Nyasa na Mkenda na itaepusha njia ya mzunguko”, amefafanua Bashungwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.